Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vyazipiga makombora manowari 3 za Marekani katika Bahari ya Sham
(last modified 2024-09-28T10:14:52+00:00 )
Sep 28, 2024 10:14 UTC
  • Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vyazipiga makombora manowari 3 za Marekani katika Bahari ya Sham

Msemaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Yemen Brigedia Yahya Saree ametangaza kuwa, katika operesheni za kijeshi zilizotekelezwa na vikosi hivyo katika Bahari ya Sham, manowari tatu za mashambulizi za Marekani zimelengwa kwa makombora na ndege zisizo na rubani wakati zikiwa njiani kwenda kutoa msaada na uungaji mkono kwa adui Mzayunii.

Saree amefafanua kwa kusema: "operesheni hiyo ilitekelezwa kwa pamoja na vikosi vya wanamaji vya makombora na vya ndege zisizo na rubani kwa kutumia makombora 23 ya balestiki na kruzi pamoja na droni moja, na kuzipiga manowari hizo za mashambulizi za Marekani (Destroyers).
 
Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen ameongeza kuwa, operesheni hiyo ya majini ni operesheni kubwa zaidi katika mapambano ya Ushindi Ulioahidiwa (Fat-hun Mauu'd) na Jihadi takatifu katika kuunga mkono Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na kutoa jibu kwa uchokozi wa pamoja wa Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen, ambayo imefanyika wakati mmoja na operesheni ya shambulio dhidi ya maeneo ya Jaffa na Ashkelon ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Makombora ya vikosi vya ulinzi vya Yemen

Vikosi vya jeshi la Yemen vimetangaza kuwa, viko tayari kutekeleza operesheni zaidi za kijeshi kwa ajili ya kuliunga mkono taifa la Palestina na Muqawama wa Lebanon.

 
Wananchi wa Yemen nao pia wametangaza uungaji mkono wao kwa operesheni za aina yake zilizotekelezwa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya utawala wa Kizayuni katika siku za hivi karibuni na kutaka kuongezwa operesheni hizo.
 
Tangu Jumatatu iliyopita, jeshi la Kizayuni limefanya mashambulizi makubwa na ya kinyama katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Lebanon na lingali linaendeleza mashambulizi hayo.
 
Zaidi ya watu 700 wakiwemo watoto zaidi 50 na wanawake zaidi ya 94 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 1,900 wamejeruhiwa tangu jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulipoanzisha mashambulio ya anga dhidi ya Lebanon.../