Hamas: Mashambulizi ya Israel hayatavuruga azma ya Yemen
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani mashambulizi ya kichokozi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Yemen na kutangaza kuwa, jinai hizo hazitazuia kuendelea uungaji mkono wa Sana'a kwa wananchi wa Palestina.
Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni mapema leo zimeshambulia maeneo kadhaa katika mji mkuu wa Yemen, Sana'a, na katika mkoa wa al Hudaidah magharibi mwa nchi hiyo.
Duru za habari za Yemen zimeripoti kuwa, raia wasiopungua 12 wameuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni leo Alhamisi katika maeneo mbalimbali nchini humo.
Kufuatia hujuma hizo za kichokozi za Israel, harakati ya Hamas imetoa taarifa ikulaani jinai za jeshi la utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya miundombinu ya Yemen hayawezi kuzuia kuendelea uungaji mkono wa serikali ya Sana'a kwa wananchi wa Palestina.
Taarifa ya Hamas imeongeza kuwa, mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Yemen ambayo yamezilenga taasisi za kiraia na miundo mbinu ya huduma za jamii mjini Sana'a na katika bandari ya al Hudaydah magharibi mwa Yemen yanazidisha hatari ya mivutani na kupanua wigo wa hujuma dhidi ya wananchi wa Palestina, Syria na nchi nyingine za Kiarabu.