Ansarullah: Matakfiri Syria ni vikaragosi vya madola ajinabi
(last modified Mon, 10 Mar 2025 11:25:06 GMT )
Mar 10, 2025 11:25 UTC
  • Ansarullah: Matakfiri Syria ni vikaragosi vya madola ajinabi

Kiongozi wa Harakati ya Muqawama ya Ansarullah ya Yemen amelaani vikali machafuko mabaya yaliyotokea hivi karibuni katika eneo la pwani ya magharibi mwa Syria na kusisitiza kuwa, mbali na kuwa ghasia hizo ni tishio kwa wahusika wa jinai hizo na walezi wao, lakini pia ni somo kwa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu.

Abdul-Malik al-Houthi aliyasema hayo katika hotuba yake iliyorushwa hewani na televisheni kutoka mji mkuu wa Yemen, Sana'a, usiku wa kuamkia leo, siku ya tisa wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Ameonya kuwa, matokeo ya ukatili huo yatakuwa makubwa kwa matakfiri wenyewe pamoja na wafadhili wao wanaodhani wako salama chini ya himaya ya Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya.

Mkuu huyo wa Ansarullah amevitaja vitendo vya jinai vinavyofanywa na makundi ya kitakfiri nchini Syria kuwa ni vya kutisha na kusisitiza kwamba ni vinapasa kulaaniwa na mtu yeyote yule.

Al-Houthi amewataka wale wote ambao bado wana dhamiri kujitahidi kukomesha uhalifu huo wa kutisha nchini Syria. Amesema Wasyria wanauawa kikatili, bila pingamizi lolote au ukosoaji kutoka kwa ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.

Wanamgambo wa kitakfiri wameuawa Wasyria zaidi ya 1,000 ndani ya wiki moja

Amesisitiza kuwa, wanamgambo wa kitakfiri wanatekeleza uhalifu wa mauaji ya halaiki dhidi ya raia wa Syria wasio na ulinzi, akisema vitendo vya unyanyasaji vilivyorekodiwa kwenye video na kusambazwa kwenye mitandao ya mitandao ya kijamii vinafichua ukatili na uhalifu wao.

Kiongozi wa Ansarullah ya Yemen amesema, "Matakfiri nchini Syria wanatumikia maslahi ya maadui wa Israel na Marekani kwa kusambaratisha mfumo wa kijamii wa Syria. Haya yanajiri wakati Wamarekani na Wazayuni wanajionyesha kuwa watetezi na waokozi wa watu wa Syria."