ICRC: Tumeshtushwa na jinsi Israel inavyofanya jinai bila ya kiwewe
Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (ICRC) limesema kuwa, limeshtushwa na jinsi utawala wa Kizayuni wa Israel unavyofanya jinai za kutisha huko Ghaza bila ya hofu wala kiwewe.
Shirika la Habari la Fars limenukuu taarifa ya jana Jumatatu ya Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ikitangaza kwamba imeshtushwa sana na uhalifu na jinai zinazofanywa na Israel baada ya kugundua miili ya wafanyakazi wanane wa misaada kutoka timu ya Hilali Nyekundu ya Palestina, wanachama watano wa Vikosi vya Ulinzi wa Raia na mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa ambao waliuawa shahidi wiki moja iliyopita katika mashambulio ya kikatili ya Israel huko Rafah, kusini mwa Ghaza.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jeshi la Israel liliyafyatulia risasi magari ya kubebea wagonjwa na magari ya misaada ya Wapalestina mjini Rafah na limekata mawasiliano na wafanyakazi wa misaada ya Kipalestina kusini mwa Ukanda wa Ghaza.
Picha za satelaiti zilizotolewa hivi karibuni zinaonyesha kuwa jeshi la Israel lilishambulia kwa uchache magari matano ya Hilali Nyekundu ya Palestina na Ulinzi wa Raia katika eneo la Tel Sultan. Picha hizo zinaonesha kuwa jeshi la Israel liliyazingira magari hayo baada ya shambulio hilo na kutoruhusu vikosi vya uokoaji kuwakaribia wahanga wa ukatili huo.
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu imesema kuwa: "Miili yao ilitambuliwa Jumapili na kuhamishiwa maeneo mengine kwa ajili ya kufanyiwa maziko ya heshima. Wafanyikazi hao na watu wa kujitolea walihatarisha maisha yao ili kusaidia watu wengine, tumesikitishwa sana na tunatoa pole kwa familia zao, wapendwa wao na wafanyakazi wenzao kwa msiba huu mkubwa."