Taasisi ya Misri yataka kuundwa kamati ya Kiislamu ya kusimamia Hija
(last modified Wed, 07 Sep 2016 13:28:45 GMT )
Sep 07, 2016 13:28 UTC
  • Taasisi ya Misri yataka kuundwa kamati ya Kiislamu ya kusimamia Hija

Taasisi moja ya nchini Misri kwa jina la "Taasisi ya Uadilifu na Ustawi wa Haki za Binadamu imezitaka nchi za Kiislamu ziasisi kamati ya Kiislamu kwa ajili ya kusimamia masuala ya Hija.

Taasisi hiyo ya Uadilifu na Ustawi wa Haki za Binadamu yenye makao yake nchini Misri imezitolea wito nchi zote za Kiislamu khususan Iran, Pakistan, Afghanistan, Indonesia, Uturuki, Chechniya na Misri yenyewe kuunda kamati kwa ajili ya kusimamia masuala ya Hija na Umra. Taasisi hiyo imetoa ujumbe huo baada ya viongozi wa Saudi Arabia kuwazuia Mahujaji wa Kiirani kushiriki katika ibada ya Hija ya mwaka huu. Taasisi ya Uadilifu na Ustawi wa Haki za Binadamu ya Misri pia imesisitiza katika ujumbe wake kuwa, nchi zote za Kiislamu zina haki ya kupanga na kusimamia masuala ya ibada ya Hija. Hii ni kwa sababu al Kaaba haimilikiwi na Saudia na viongozi wa nchi hiyo pekee, bali ni mali ya Waislamu wote wa dunia nzima.

Taasisi hiyo imeashiria kushindwa Saudi Arabia kudhamini usalama na ulinzi wa mahujaji katika hija ya mwaka jana na kusisitiza kuwa, kuwepo udhaifu katika kusimamia ibada hiyo na kuwepo msongamano mkubwa wa mahujaji kupita kiasi kulisababisha kuaga dunia mahujaji wengi wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu. Taasisi ya Uadilifu na Ustawi wa Haki za Binadamu ya Misri pia imeashiria shambulio la kigaidi la hivi karibuni karibu na Masjidul Nabii na kueleza kuwa, viongozi wa Saudia  hata wameshindwa kuzuia kutekelezwa shambulio la kigaidi karibu na msikiti huo huku wakiwatwisha Mahujaji masharti yasiyofaa na kuyazuia mataifa mengine ya Kiislamu kushiriki katika ibada ya Hija.

Mahujaji walioaga dunia mwaka jana katika maafa ya Mina

 

Tags