Jeshi la Syria laendelea kupata mafanikio makubwa dhidi ya magaidi wakufurishaji
Jeshi la Syria kwa kushirikiana na wanamapambano limeendelea kusonga mbele katika maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na wanachama wa makundi ya kigaidi na kitakfiri.
Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo imesema kuwa, askari wa serikali na wale wa muqawama wa Hizbullah wameendelea kusonga mbele na kuyakomboa maeneo ya kusini mwa mkoa wa Aleppo, kaskazini mwa nchi hiyo sanjari na kushadidisha mzingiro dhidi ya magaidi. Katika operesheni hizo, idadi kubwa ya magaidi wameangamizwa huku zana zao za kijeshi zikidhibitiwa na zingine kuharibiwa.
Kabla ya hapo jeshi la wananchi nchini Syria lilidhibiti kiwanda cha gesi, majengo na kituo cha upekuzi katika eneo la al-Ramusa kusini mwa mkoa wa Aleppo kutoka mikononi mwa magenge ya kigaidi. Aidha siku chache zilizopita, jeshi la nchi hiyo sanjari na kudhibiti kikamilifu chuo kidogo na batalioni ya kijeshi kusini mwa mkoa huo, liliwazingira magaidi katika eneo la mashariki mwa Aleppo. Wakati huo huo kanali ya Kiarabu ya al-Mayadin imeripoti kuuawa mamia ya magaidi katika mapigano na jeshi la Syria na kadhalika mashambulizi ya anga ya jeshi la serikali ya nchi hiyo na Russia dhidi ya maeneo ya magaidi hao katika mikoa ya Aleppo na Idlib, kaskazini na kaskazini magharibi mwa Syria.