Daesh yaendeleza jinai zake, yachinja mabarobaro 17 Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i1564-daesh_yaendeleza_jinai_zake_yachinja_mabarobaro_17_iraq
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limeua vijana 17 kwa kuwakata vichwa katika mkoa wa Kirkuk, kaskazini mwa Iraq.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 19, 2016 23:37 UTC
  • Daesh yaendeleza jinai zake, yachinja mabarobaro 17 Iraq

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limeua vijana 17 kwa kuwakata vichwa katika mkoa wa Kirkuk, kaskazini mwa Iraq.

Sheikh Anwar al-Aasi, kiongozi wa kabila la al-Ubaid amesema matakfiri hao wa Daesh wamewachinja vijana 17 katika mji wa Hawijah, yapata kilomita 280 kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Baghdad. Kanali ya televisheni inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kiarabu ya al-Sumaria imeripoti kuwa, magaidi hao wametekeleza mauaji hayo ya kikatili dhidi ya vijana 17, kwa kuwatuhumu kuwa waliandika mabango yaliyokuwa na ujumbe wa kulikashifu kundi hilo la kitakfiri.

Siku chache zilizopita kundi hilo la kigaidi liliwanyonga raia zaidi ya elfu moja katika mji wa Mosul huko Iraq, na baadaye kuzika miili yao katika makaburi ya umati huko kusini magharibi mwa mji huo. Kadhalika mwezi Aprili mwaka jana, kundi la kigaidi la Daesh liliwanyonga wakazi karibu 2100 wa mji wa Mosul. Kundi hilo la kigaidi likiungwa mkono na baadhi ya nchi za Magharibi na za Kiarabu liliingia nchini Iraq yapata miaka miwili iliyopita na kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ukiwemo mji wa Mosul na kutenda jinai za kutisha.