Marekani; mwongozaji wa njama dhidi ya Syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid al-Muallem amesema Marekani ndiyo iliyoshika usukani wa njama inayotekelezwa dhidi ya nchi yake; na nchi nyingine za Magharibi na za eneo la Mashariki ya Kati zinaisaidia Washington katika kufanikisha njama hiyo.
Walid al-Muallem ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya habari ya al-Mayadeen ya Lebanon na akabainisha kuwa Marekani imewasheheni magaidi kwa silaha, inawasaidia kifedha na inaingiza maelfu ya magaidi nchini Syria kupitia mipakani mwa nchi hiyo.
Al-Muallem amesisitiza kuwa kama Marekani ina nia ya kweli ya kutatua mgogoro wa Syria ikomeshe misaada na uungaji mkono wake kwa makundi ya kigaidi; uungaji mkono ambao unatekelezwa na nchi tiifu kwa Washington katika eneo hili.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria uungaji mkono wa Marekani na nchi nyingine kwa magaidi nchini Syria ungali unaendelea; na misaada hiyo inawafikia magaidi hao kupitia mpaka wa Uturuki.
Mbali na kuashiria kwamba Marekani haikuheshimu makubaliano yake na Ruissia kuhusu kutofautisha makundi ya upinzani yenye misimamo ya wastani na kundi la kigaidi na kitakfiri la Jabhatu-Nusrah (Fat-h Sham), Al-Muallem amesema, mashambulio yaliyofanywa na Marekani Deir Az Zor na kuwalenga makusudi askari wa jeshi la Syria kumedhihirisha wazi hakika ya malengo ya Washington siku mbili kabla ya kumalizika muda wa usitishaji vita.
Majimui ya mwenendo na vitendo vya Marekani na washirika wake kuhusiana na mgogoro wa Syria vinathibitisha ukweli wa maelezo yaliyotolewa na Walid al-Muallem katika mahojiano yake na al-Mayadeen. Mgogoro wa Syria ulizuka katika vuguvugu la mapinduzi ya wananchi katika eneo, lakini haukuwa na sura inayofanana na mapinduzi hayo.
Mwenendo wa Marekani mara baada ya kuzuka mgogoro wa Syria umeonyesha kuwa tangu mwanzo kulikuwa na njama iliyoratibiwa dhidi ya mrengo wa mstari wa mbele wa mhimili wa muqawama katika eneo. Ukweli ni kwamba Syria, ambayo ni ngome muhimu ya mhimili wa muqawama dhidi ya Uzayuni, ni mwiba uliowakwama kooni Wazayuni maghasibu; na hatua za kila aina zilizochukuliwa kwa lengo la kuisambaratisha ngome hiyo zinazidi kuonyesha hali tata zilizogubika anga ya mgogoro wa Syria. Madai ya Magharibi na hasa Marekani ya kuunga mkono demokrasia nchini Syria na kuwahurumia raia wa nchi hiyo ni hila tu ya kutaka kuwahadaa walimwengu; na nyuma yake imejificha njama chafu inayotekelezwa dhidi ya nchi hiyo.
Kama Marekani ingekuwa kweli inajali uhuru na haki za binadamu isingeandaa mazingira kwa maelfu ya magaidi makatili, washenzi na wauaji kumiminika nchini Syria na kufanya mauaji ya kinyama ya halaiki dhidi ya wanawake, watoto na wazee wasio na hatia. Kutaka kuwatwisha demokrasia Wasyria kupitia jinai za magaidi kunazidi kuweka wazi ukweli kwamba kile kinachoitwa mgogoro wa Syria si kingine bali ni njama chafu iliyopangwa na kutekelezwa dhidi ya nchi hiyo.
Inafaa tujiulize; kuuawa Wasyria wapatao laki tatu, kuteketezwa miundombinu ya Syria, kubaki bila makaazi mamilioni ya raia wa nchi hiyo na kulazimika kufanya safari ya uhajiri yenye chungu ya hatari, mashaka na mateso ndio gharama ya kupata utawala wa kidemokrasia ambao Marekani na waungaji mkono wake wanadai kuwa ndicho wanachokihangaikia kwa mwaka wa tano na nusu sasa kwa ajili ya nchi hiyo?
Huruma za mamba zinazoonyeshwa na Marekani, Uturuki, Saudi Arabia, Uingereza na Ufaransa kwa wananchi wa Syria kupitia vikao mbalimbali vinavyoitishwa kwa jina la eti 'marafiki' wa Syria huko New York na kwengineko na hatua ya siku ya Jumapili iliyopita ya kuitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, yote hayo hayana lengo jingine isipokuwa kuzibabaisha fikra za walimwengu ili kufanikisha malengo yao nchini Syria.../