Milipuko ya mabomu yaua zaidi ya 20 Syria
Habari za hivi punde zinasema kuwa watu wasiopungua 20 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia milipuko miwili ya mabomu katika mkoa wa Homs, magharibi mwa Syria.
Habari zaidi zinasema kuwa, milipuko hiyo imetokea katika eneo la Zahra lenye shughuli nyingi. Duru za hospitali zinasema huenda idadi ya vifo ikapanda kutokana na majeruhi wengi kuwa katika hali mbaya. Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na hujuma hiyo lakini dalili za awali zinaonyesha huenda magaidi wa Daesh ndio waliohusika. Kundi hilo la kigaidi na kitakfiri limehusika na mashambulizi ya aina hiyo katika siku za huko nyuma. Serikali ya Syria imelaani shambulizi la leo na kuahidi kushadidisha mashambulizi yake dhidi ya ngome za magaidi katika maeneo yote ya nchi hiyo. Umoja wa Mataifa pia umetoa kauli ya haraka kulaani mauaji hayo ya raia wasio na hatia.