Makumi ya maelfu ya watu waukimbia mkoa wa Nainawa, Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i18880-makumi_ya_maelfu_ya_watu_waukimbia_mkoa_wa_nainawa_iraq
Kamati ya Wahajiri ya Bunge la Iraq imetangaza kuwa, karibu watu 29 elfu wameukimbia mkoa wa Nainawa tangu ilipoanza operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul, makao makuu ya mkoa huo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Nov 05, 2016 23:14 UTC
  • Makumi ya maelfu ya watu waukimbia mkoa wa Nainawa, Iraq

Kamati ya Wahajiri ya Bunge la Iraq imetangaza kuwa, karibu watu 29 elfu wameukimbia mkoa wa Nainawa tangu ilipoanza operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul, makao makuu ya mkoa huo.

Shirika la habari la Sumaria News la nchini Iraq, limemnukuu Raad al Dehlaki, mkuu wa kamati hiyo akisema jana (Jumamosi) kuwa, kuna uwezekano idadi ya wakimbizi hao ikaongezeka katika siku zijazo kutokana na kuzidi kuingia wanajeshi wa Iraq katikati ya mji wa Mosul.

Al Dehlaki ametahadharisha kuwa, Wizara ya Wahajiri ya Iraq ina uwezo wa kupokea wakimbizi laki moja tu kutoka Mosul na kuitaka Wizara ya Fedha ya nchi hiyo hiyo kutoa fedha za kutosha za kuwahudumia wakimbizi zaidi ili kuepusha janga la kibinadamu.

Wakimbizi wa Iraq wanaokimbia mapigano mkoani Nainawa

 

Wakati huo huo vikosi vya jshi la Iraq jana (Jumamosi) viliingia katika mji wa Hamam al Alil, kusini mwa Mosul na kupandisha bendera ya nchi hiyo juu ya majengo ya mji huo.

Opereseheni ya kuukomboa mji wa Mosul iliianza tarehe 17 mwezi uliopita wa Oktoba na hadi hivi sasa karibu vijiji 150 vimeshakombolewa kutoka mikononi mwa genge la kigaidi la Daesh.

Si hayo tu, lakini pia kamanda wa jeshi la Iraq katika mkoa wa Nainawa nchini Iraq, Abdul Amir Rashid Yarullah, ametangaza kuwa jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na harakati ya wananchi, limefanikiwa kukomboa wafungwa 45 waliokuwa wanashikiliwa na genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) magharibi mwa Mosul.