HRW: Daesh wanatumia silaha za kemikali wakikimbia Mosul
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh wanatumia silaha za kemikali kaskazini mwa mji wa Mosul nchini Iraq.
Lama Fakih, Naibu Mkurugenzi wa shirika hilo eneo la Mashariki ya Kati amesema magaidi hao wanatumia silaha hizo hatari wakikimbia mji huo ambao kwa sasa unashuhudia makabiliano makali kati yao na vikosi vya serikali.
Kwa mujibu wa Human Rights Watch, wanamgambo hao wa Daesh wametekeleza mashambulizi matatu ya silaha za kemikali katika mji wa Qayyarah, kusini mwa Mosul.
Hii ni katika hali ambayo, siku chache zilizopita, vikosi vya serikali ya Iraq viligundua kaburi la umati karibu na mji wa Mosul. Brigedia Jenerali Yahya Rasool, msemaji wa Komandi ya Pamoja ya Vikosi vya Iraq amesema kuwa, kaburi hilo la umati limepatikana likiwa na miili 100 katika mji wa Hammam al-Alil, yapata kilomita 14 kusini mwa Mosul.
Askari wa jeshi la serikali kwa kushirikiana na harakati ya wananchi ya Hashdu Sha'abi wamesonga mbele katika eneo la Hamam al-Alil, kusini mwa mji wa Mosul na kukomboa kikamilifu vijiji kadhaa kikiwemo Qabr al-Abd pamoja na mji wa kihistoria wa Nimrud, kutoka mikononi mwa wanachama wa kundi hilo la wakufurishaji.