Hizbullah yasisitiza kuendeleza mapambano dhidi ya magaidi hadi kuwaangamiza kikamilifu
Harakati ya Mapambano ya Hizbullah ya Lebanon imesisitiza juu ya kuendeleza mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi na kitakfiri na kuyatokomeza kikamilifu.
Taarifa iliyotolewa na Hizbullah sambamba na kulaani shambulio la kigaidi la jana la kundi la kigaidi la Daesh mjini Hilla Iraq dhidi ya Mazuwwar imebainisha kuwa, harakati hiyo itaongeza juhudi zake zenye lengo la kung'oa mizizi ya magaidi na kuwazuia kufikia malengo yao.
Harakati ya Mapambano ya Hizbullah imetoa wito pia wa kukomeshwa siasa za ulipizaji kisasi za madola makubwa ya kimataifa na ya kieneo.
Sehemu moja ya taarifa hiyo ya Hizbullah ya Lebanon imeeleza kuwa, jinai ya jana ya kundi la kigaidi la Daesh mjini Hilla Iraq ni mwendelezo wa jinai za kigaidi na za kimauaji zinazofanywa na makundi yasiyo na dini wala hekima ambayo yamekuwa yakimwaga damu za watu waumini na wasio na hatia.
Hizbullah imesema kuwa, makundi hayo yanafanya jinai hizo ili kupoza chuki na vinyongo vyao walivyovificha nyuma ya pazia la madai ya kidini.
Mlipuko wa jana wa gari lililokuwa limetegwa mabomu katika kituo cha mafuta ya petroli katika eneo moja mjini Hilla nchini Iraq uliua shahidi karibu Waislamu 100 waliokwenda kufanya ziara ya Imam Hussein as na kujeruhi wengine zaidi ya 20. Makumi ya mashahidi waliouawa katika shambulio hilo la kigaidi ni raia wa Iran.