Viongozi wa kundi la Daesh watoroka mji wa Mosul
Vyombo vya kuaminika katika mkoa wa Nineveh huko kaskazini mwa Iraq vimeripoti kuwa, makamanda wa kundi la Daesh akiwemo kiongozi wa kundi hilo, Abu Bakar al Baghdadi, wameukimbia mji wa Mosul na kuelekea katika maeneo ya mpaka wa Iraq na Syria.
Ripoti zinasema kuwa, baada ya amri ya viongozi wa kundi la Daesh ya kuwataka wanachama wa kundi hilo kuondoka Mosul kufuatia kushindwa mara kwa mara na kuzidi kuzingirwa na jeshi la Iraq, kiongozi wa kundi hilo Abu Bakar al Baghdad na maafisa wengine wa kundi hilo wamejificha katika eneo la al Biaj kwenye mpaka wa nchi hiyo na Syria.
Kamanda wa operesheni ya kukomboa Mosul, Najm al Jabouri ameashiria mparaganyiko uliojitokeza katika safu za magaidi wa Daesh na kushindwa kuendelea na mapigano na kusema kuwa: Mji wa Mosul utakuwa umekombolewa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Operesheni ya kukomboa Mosul ilianza tarehe 17 Oktoba kutokea maeneo sita tofauti na katika siku za hivi karibuni jeshi la Iraq likishirikiana na makundi ya kujitolea ya wananchi, limefanikiwa kuingia katika vitongoji na viunga vya mji huo uliokuwa ngome kuu ya kundi la kikati na kigaidi la Daesh kwa miaka kadhaa.