HRW: Watu 133 wamepokonywa uraia nchini Bahrain mwaka jana 2016
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema makumi ya raia wa Bahrain walivuliwa uraia na serikali mwaka uliopita 2016.
Laila Matar, Mwanasheria wa HRW mjini Geneva ameiambia kanali ya televisheni ya Lualua inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kiarabu kuwa, shirika hilo la kimataifa limerekodi visa 133 vya raia wa Bahrain kupokonywa uraia na serikali kwa kuukosoa utawala huo wa Aal-Khalifa.
Kadhalika afisa huyo wa Human Rights Watch amekosoa mwenendo wa serikali ya Manama kuwapandisha kizimbani raia wa nchi hiyo katika mahakama za kijeshi.
Mwaka jana, Mahakama ya Jinai ya Bahrain iliwavua uraia wananchi kadhaa kwa tuhuma za kujiunga na Muungano wa Februari 14 wa vijana wanaoupinga utawala wa kidikteta wa Aal-Khalifa.
Kadhalika, Utawala wa kizazi cha Aal Khalifa nchini Bahrain uliendeleza ukiukaji wake mkubwa wa haki za binadamu kwa kumnyang'anya uraia mwanazuoni mkubwa na mashuhuri wa Kiislamu nchini humo Ayatullah Issa Ahmad Qasim.
Mamia ya wanaharakati wa masuala ya kijamii na kisiasa wameswekwa jela nchini humo kwa tuhuma zisizo na msingi na wengine wamekuwa wakinyang'anywa uraia ili kuwafunga midomo.