Apr 12, 2017 08:05 UTC
  • Udharura wa kutatuliwa haraka mgogoro wa wakimbizi wa Palestina

Kamishna wa Wakala wa Umoja wa Mataifa wa Misaada na Kazi kwa Wakimbizi wa Palestina UNRWA umetaka mgogoro wa wakimbizi wa Palestina walioenea katika kona zote za dunia, utatuliwe haraka.

Pierre  Krähenbühl amesema hayo mbele ya wanachuo wa Taasisi ya Mawasiliano ya Kimataifa mjini Moscow, Russia na kuongeza kuwa, zaidi ya wakimbizi milioni 5 wa Palestina hivi sasa wanateseka kutokana na kuzingirwa, kutekwa maeneo yao, kukosa makazi na vita, hivyo jamii ya kimataifa ina jukumu la kutafuta njia ya kiuadilifu na ya kudumu ya kutatua kikamilifu matatizo ya wakimbizi wa Palestina.

Kamishna huyo wa UNRWA aidha amesema, wakimbizi wa Palestina hawapaswi kusahauliwa akisisitiza kuwa, misaada ya kifedha ya nchi mbalimbali za dunia ikiwemo Russia kwa wakimbizi hao inaonesha kuwa walimwengu wanatambua rasmi haki za wakimbizi wa Palestina. Utawala wa Kizayuni unafanya njama za kila namna za kujaribu kulisahaulisha suala la wakimbizi wa Palestina kama vile kutaka wakimbizi hao wapewe makazi huko huko walikokimbilia na wasiruhusiwe kurejea Palestina.

Njama nyingine zinazofanywa na Israel ni kujaribu kuteka ardhi zote za Palestina na hivyo kuondoa fursa ya aina yoyote ya kurejea wakimbizi hao katika ardhi za mababu zao. Hii ni katika hali ambayo azimio 194 la Umoja wa Mataifa linabainisha wazi kwamba ni haki ya wakimbizi wa Palestina kurejea katika nchi yao kama ambavyo utawala wa Kizayuni nao una wajibu wa kuwalipa gharama zote wakimbizi hao kutokana na hasara ulizowasababishia.

Zaidi ya Wapalestina milioni tano na nusu ni wakimbizi katika maeneo tofauti duniani kwa zaidi ya miongo sita kutokana na jinai za Israel na kutekwa kidhulma ardhi zao na utawala ghasibu wa Kizayuni. Nchi za Magharibi hususan Marekani na Uingereza ni waungaji mkono wakuu wa jinai za Wazayuni huko Palestina kama ambavyo nchi hizo za kibeberu zinaunga mkono pia mipango ya Israel ya kuvuruga muundo wa kijamii wa maeneo ya Wapalestina na kuyayahudisha maeneo hayo. Kwa hakika miongoni mwa jinai kubwa zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na Israel na waitifaki wake ni kuwafanya watu milioni tano na nusu kuwa wakimbizi baada ya kuporwa kila kitu chao zikiwemo ardhi za mababu zao. Matamshi yanayotolewa na maafisa wa Umoja wa Mataifa wakiwemo wale wa taasisi ya UNRWA kwa hakika ni radiamali dhidi ya wimbi jipya la juhudi za Marekani za kujaribu kufufua mazungumzo ya mapatano kwa shabaha ya kuwapora kikamilifu Wapalestina haki zao zote. Hivi sasa serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani inaandaa mpango wa kukamilisha njama za huko nyuma za Marekani na tawala za nchi za Magharibi dhidi ya taifa madhlumu la Palestina. 

Bendera ya utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Kimsingi mchakato wa mazungumzo ya mapatano ya Mashariki ya Kati ambayo yalianza mwaka 1991 kwa kubuniwa na kuongozwa na Marekani na tawala za nchi za Magharibi, ni mchakato hatari na tata mno ambao lengo lake ni kuwapoka kikamilifu Wapalestina haki zao zote zilizobakia. Mhimili mwingine wa njama za Marekani katika eneo hili ni mpango wa mapatano wa Kiarabu uliopendekezwa na Saudi Arabia mwaka 2002. Kudharauliwa kikamilifu suala la wakimbizi na mateka wa Kipalestina katika mpango huo wa Saudi Arabia, ni sehemu ndogo tu ya madhara na hatari za mpango huo ambao unaonekana unataka kuukabidhi kila kitu utawala wa Kizayuni na kutowabakishia chochote Wapalestina. Amma radiamali ya Umoja wa Mataifa dhidi ya njama za kutaka kuwapora Wapalestina haki zao inaonesha kushindwa njama za maadui wa taifa lililodhulumiwa mno la Palestina.

Tags