Watetezi: Bahrain inakiuka haki ya faragha na uhuru wa kujieleza
Shirika moja la kutetea haki za binadamu nchini Bahrain limeelezea wasiwasi kuhusu hatua ya utawala wa Aal-Khalifa kuendelea kukandamiza haki ya faragha na uhuru wa kujieleza wa wananchi wa nchi hiyo.
Taarifa ya Bahrain Center for Human Rights imesema kuwa, watawala wa nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi wamebuni vikwazo vipya eti vya kiusalama, vinavyohujumu faragha ya watu katika mitandao ya kijamii. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Wizara ya Elimu ya Bahrain siku chache zilizopita iliwaagiza walimu wakuu wa shule zote za upili kuchunguza jumbe zilizotumwa hivi karibuni katika makundi ya mtandao wa kijamii wa Watsapp ya walimu na wanafunzi.
Hii ni katika hali ambayo, mapema jana, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al-Hussein, kwa mara nyingine tena alilaani ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Aal-Khalifa dhidi ya wananchi wa Bahrain na kusema kuwa, serikali ya Manama imedhihirisha namna isivyoheshimu haki za watetezi wa haki nchini humo.
Kadhalika afisa huyo wa UN alivitaka vyombo vya mahakama kukomesha tabia ya kutoa hukumu zisizo za kiadilifu dhidi ya raia wa nchi hiyo na haswa hukumu ya kuwapokonya uraia wananchi wake wanaoonekana kuukosoa utawala huo wa kifalme.