Jun 07, 2017 07:13 UTC
  • Saudia kuwanyonga Mashia 14 kwa kushiriki maandamano, HRW yalaani

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema utawala wa Aal-Saud umepanga kuwanyonga wanaharakati 14 wa Kishia eti kwa kosa la kushiriki maandamano.

Sarah Leah Whitson, Mkurugenzi Mkuu wa Human Rights Watch katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika amesema kiwango cha watu kuhukumiwa kifo nchini Saudi Arabia kinatia wasi wasi mkubwa kwa kuwa Riyadh inatumia hukumu hizo kukandamiza wapinzani na wakosoaji wake, kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kuimarisha usalama wa taifa.

Wakati huo huo,Lynn Maalouf, Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International eneo la Mashariki ya Kati amesema mchakato wa kesi zilizopelekea kutolewa hukumu hizo za vifo umekiuka wazi wazi viwango vya kimataifa vya kutolewa hukumu za kiadilifu. 

Hukumu ya kifo kwa kukatwa kichwa Saudia

Tangu tarehe 10 ya mwezi uliopita wa Mei, askari wa vikosi vya usalama vya utawala wa Aal Saud wamekuwa wakifanya mashambulio dhidi ya eneo la Waislamu wa madhehebu ya Shia la Al-A'wamiyyah kwa sababu wanalichukulia eneo hilo kuwa kitovu cha harakati za upinzani na malalamiko dhidi ya utawala huo wa kifalme.

Mwaka jana pekee, utawala wa Aal-Saud uliwanyonga watu 153, akiwemo Sheikh Nimr Baqir al-Nimr, msomi mashuhuri wa Kishia, hatua iliyokabiliwa na wimbi kubwa la malalamiko kutoka nchi mbalimbali hususan katika ulimwengu wa Kiislamu.

Tags