Kuongezeka operesheni ya vikosi vya Iraq dhidi ya Daesh
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i3040-kuongezeka_operesheni_ya_vikosi_vya_iraq_dhidi_ya_daesh
Baada ya kuzingirwa eneo la kiistratejia la Hit katika mkoa wa al-Anbar magharibi mwa Iraq, Spika wa Bunge la nchi hiyo amesema kuwa, mkoa huo utakombolewa wote kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh katika siku chache zijazo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 14, 2016 09:48 UTC
  • Kuongezeka operesheni ya vikosi vya Iraq dhidi ya Daesh

Baada ya kuzingirwa eneo la kiistratejia la Hit katika mkoa wa al-Anbar magharibi mwa Iraq, Spika wa Bunge la nchi hiyo amesema kuwa, mkoa huo utakombolewa wote kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh katika siku chache zijazo.

Akiwa katika safari yake katika mkoa wa al-Anbar hapo jana Jumapili Salim al-Jabouri Spika wa Bunge la Iraq aliashiria kukombolewa mji wa Ramadi ambao ni makao makuu ya mkoa wa al-Anbar na kuzingirwa maeneo ya kiistratejia kama Fallujah na Hit sambamba na kuanza duru mpya ya operesheni ya vikosi vya wananchi na jeshi katika mkoa huo na kusema kuwa, katika siku chache zijazo kutashuhudiwa kukombolewa mkoa huo kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh. Jeshi la Iraq limethibitisha kuzingirwa eneo la Hit lililoko magharibi mwa Ramadi na kutangaza kuwa, magaidi wa Daesh wameondoka magharibi mwa al-Anbar na sasa wamo katika harakati za kukimbilia katika mipaka ya Syria.

Kwa mujibu wa ripoti ya Baraza la Mkoa wa al-Anbar makumi ya magaidi wa Daesh waliuawa katika operesheni ya juzi katika mkoa wa al-Anbar. Kundi la kigaidi la Daesh jana liliwanyonga wanachama wake 35 ambao waliasi na kukataa kukabiliana na vikosi vya wananchi na vya jeshi la Iraq. Maafisa wa serikali ya Iraq wanasema kuwa, baada ya magaidi wa Daesh kupata pigo katika miezi ya hivi karibuni kwenye maeneo mbalimbali ya Iraq kama vile katika mikoa ya al-Anbar NA Swalahuddeen wameongeza mashinikizo dhidi ya wapiganaji wao na vitendo vya jinai katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo hususan vitendo vya utegaji mabomu katika mji mkuu Baghdad.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, vipigo mfululizo walivyopata wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh na kukaribia kushindwa na jeshi la Iraq ndiyo mambo yaliyowafanya wapiganaji wake wachanganyikiwe na kuanza kufanya hujuma za kigaidi za kiholela kwa kutega mabomu yanayouwa watu wasio na hatia yoyote. Kitendo cha wanamgambo wa Daesh cha kutumia silaha za kemikali ni jinai nyingine zinazoongezwa katika faharasa ndefu ya jinai za wanamgambo hao huko Iraq. Haider al-Abadi, Waziri Mkuui wa Iraq ameyataja mashambulio ya kemikali ya Daesh kuwa ni maafa na kutangaza kuwa, vikosi vya nchi hiyo vitatoa jibu kali kwa jinai hizo za magaidi wa Daesh.

Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa watu 670 wameuawa katika mashambulizi ya kigaidi nchini Iraq kwenye mwezi uliopita wa Februari pekee. Takwimu zilizotolewa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq zinaonesha kuwa, Wairaqi 670 wameuawa mwezi uliopita wa Februari na wengine 1,290 kujeruhiwa katika mashambulizi ya kigaidi.

Kundi la kigaidi la Daesh liliteka maeneo mengi ya kaskazini na magharibi mwa Iraq mwezi Juni mwaka 2014 ambapo sanjari na kutenda jinai nyingi dhidi ya wananchi wa nchi hiyo, limefanya uharibifu mkubwa dhidi ya maeneo ya kihistoria, kidini na turathi za kiutamaduni zenye thamani kubwa za nchi hiyo. Hata hivyo hivi sasa jeshi na vikosi vya wananchi huko Iraq vimefanikiwa kukomboa maeneo muhimu kutoka kwa kundi hilo la kigaidi na kila leo habari zinaonesha kuzidi kuelemewa kundi hilo la kitakfiri.