HRW: Sasa Marekani ikomeshe uungaji mkono wake kwa Saudi Arabia
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) amesisitizia wajibu wa kusitishwa uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Saudi Arabia.
Kenneth Roth amekosoa uungaji mkono wa Washington kwa utawala wa Saudia na kuandika kuwa, Marekani inapaswa kuacha kuuunga mkono utawala wa Aal Saud.
Ameongeza kuwa Marekani inaupatia silaha utawala wa Saudia ambao unazitumia kuwaulia raia wa Yemen. Mkurugenzi Mtendaji wa Human Rights Watch amesisitiza kuwa, Rais wa Marekani, Donald Trump anapaswa kukomesha uuzaji silaha wa nchi hiyo kwa Saudi Arabia. Akiwa katika ziara mjini Riyadh hivi karibuni, Donald Trump alisaini makubaliano ya kuiuzia Saudia silaha na zana za kisasa za kijeshi zenye thamani ya dola bilioni 110.
Saudi Arabia ikisaidiwa na Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi ilianzisha uvamizi wa kijeshi nchini Yemen mwezi Machi mwaka juzi; mashambulizi ambayo yameshauwa maelfu ya wanawake na watoto wa Yemen wasio na hatia.
Hii ni katika hali ambayo Shirika la Msamaha Duniani Amnesty International na Baraza la Haki za Binadamu zimeashiria hatua ya Uingereza, Marekani na Ufaransa ya kuipatia Saudi Arabia silaha ili kuzitumia katika uvamizi wake dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Yemen na kulaani vikali kitendo hicho.