Trump kumaliza ushirikiano wa CIA na magaidi wa Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i32016-trump_kumaliza_ushirikiano_wa_cia_na_magaidi_wa_syria
Serikali ya rais wa Marekani, Donald Trump imeamua kumaliza miaka kadhaa ya ushirikiano wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA na magenge ya kigaidi nchini Syria ambayo Wamarekani wanadai ni wapinzani wenye misimamo ya wastani wanaopigana na serikali ya Rais Bashar al Assad. Shirika la Kijasusi la Marekani limekuwa likiyapa silaha na mafunzo ya kijeshi magenge hayo kwa miaka kadhaa sasa.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jul 20, 2017 03:21 UTC
  • Trump kumaliza ushirikiano wa CIA na magaidi wa Syria

Serikali ya rais wa Marekani, Donald Trump imeamua kumaliza miaka kadhaa ya ushirikiano wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA na magenge ya kigaidi nchini Syria ambayo Wamarekani wanadai ni wapinzani wenye misimamo ya wastani wanaopigana na serikali ya Rais Bashar al Assad. Shirika la Kijasusi la Marekani limekuwa likiyapa silaha na mafunzo ya kijeshi magenge hayo kwa miaka kadhaa sasa.

Gazeti la Washington Post limewanukuu maafisa wawili wa Marekani bila ya kutaja majina yao wakisema kuwa, hatua ya kusimamishwa mpango huo iliripotiwa jana Jumatano. Hata hivyo CIA imekataa kusema lolote kuhusu suala hilo.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani White House, Bi Sarah Sanders naye amekataa kusema lolote kuhusu habari hiyo. Misaada ya Shirika la Kijasusi la Marekani CIA kwa magenge ya waasi nchini Syria inadaiwa kuanza kutolewa mwaka 2013 kama njama za Barack Obama za kutaka kumpindua Rais Bashar al Assad, hata hivyo misaada hiyo imefeli.

Magaidi wanaosaidiwa na Marekani nchini Syria

Pigo jingine kwa mpango huo wa CIA ni kuwa, baadhi ya waasi hao wamejiunga na genge hatari la kigaidi la Daesh na magenge mengine yanayofanya jinai ndani na nje ya Syria.

Maafisa hao wa Marekani wamesema, hatua ya Trump ya kufunga mpango huo inaonekana ni katika juhudi zake za kuwa na uhusiano wa karibu na Russia.

Mmoja wa maafisa hao amenukuliwa na gazeti hilo la Washington Post akisema: "Hii ni ishara ya wazi kwa Putin kwamba serikali ya hivi sasa ya Marekani inataka kuboresha uhusiano wake na Russia."

Maafisa hao wameongeza kuwa, uamuzi wa kufunga ushirikiano wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA na waasi wa Syria ulichukuliwa mwezi mmoja uliopita, kabla ya rais wa Marekani kuonana na rais wa Russia pambizoni mwa kikao cha G20 nchini Ujerumani. Vile vile wamesema, hatua hiyo si sehemu ya mazungumzo ya Marekani na Russia kuhusiana na kusitishwa vita kusini magharibi mwa Syria.