Jul 25, 2017 09:22 UTC
  • Mashia wa Saudi Arabia, wahanga wa panga la Aal Saud

Mahakama za Saudi Arabia imewahukumu kifo Waislamu 29 wa madhehebu ya Shia nchini humo.

Waislamu hao wa Kishia waliohukumiwa kifo ni wakazi wa miji ya Qatif, Al-Ahsa na mji mtakatifu wa Madina.

Hata hivyo hukumu hiyo ya kifo imekosolewa sana na jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu ambazo zimeitaja kuwa ni kielelezo cha ukiukaji mkubwa wa vigezo na sheria za kimataifa. Kwanza ni kuwa, hukumu hizo za kifo dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia huko Saudi Arabia ni dhihirisho la ubaguzi wa kimadhehebu unaoendelea kufanywa na utawala wa Saudi Arabia ambao umekuwa ukiwapiga vita waziwazi Waislamu wanaofuata madhehebu ya Shia. Hii ni pamoja na kuwa, miongoni mwa misingi mikuu ya sheria za haki za binadamu ni kupiga marufuku ubaguzi wa aina zote sawa uwe wa kidini, kimadhehebu, kikabila, kimbari na kadhalika. Si hayo tu, bali tunaweza kusema kuwa, marufuku ya ubaguzi ni miongoni mwa misingi mikuu na muhimu ya haki za binadamu ambayo haipasi kukiukwa na kuvunjwa.

Raia wanahukumiwa kifo kwa kushiriki katika maandamano ya amani Saudi Arabia

Pili ni kwamba, hukumu za kifo zinazotolewa na mahakama za Saudi Arabia zikiwemo hukumu za vifo dhidi ya Waislamu 29 wa madhehebu ya Shia ni kielelezo cha mauaji ya halaiki. Hii ni pamoja na kuwa, mauaji ya halaiki ni miongoni mwa jinai kubwa zinazosanifiwa na kuwekwa kwenye orodha ya jinai dhidi ya binadamu.

Tatu ni kwamba, kwa kuzingatia kuwa, hukumu za vifo zilizotolewa na mahakama za Saudi Arabia dhidi ya raia hao wa madhehebu ya Shia hazina msingi na mashiko ya kisheria, na kimsingi watu wanaohukumiwa kifo hawajatenda jinai na uhalifu, kutolewa kwa hukumu hizo ni ukiukaji wa haki maarufu ya kuishi unaofanywa na utawala wa kifalme wa Saudia. Haki ya kuishi ni miongoni mwa misingi muhimu ya haki za binadamu ambayo haipaswi kukaganyagwa au kupuuzwa na nchi au upande wowote.

Ili kuhalalisha hukumu hizo za vifo, utawala wa Saudi Arabia umetoa madai ya changamoto za kiusalama, wakati watu hao waliohukumiwa kifo hawakutishia usalama wa taifa bali walishiriki katika maandamano ya amani ya kupinga ubaguzi katika muundo wa kibaguzi wa utawala wa nchi hiyo. Kwa hakika tunaweza kusema kuwa, utawala wa Saudia unatekeleza mauaji ya kisiasa dhidi ya watu ambao hawakuhusika na uhalifu wa kisiasa.

Mbinu za Mawahabi za kuua Waislamu zinashabihiana, Saudia na Daesh

Kwa kutilia maanani ukweli huo wachambuzi na weledi wa masuala ya siasa za Saudi Arabia wanasema kuwa, Aal Saud wanatumia hukumu ya kifo kama silaha ya kisiasa dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo. Katika uwanja huo Mkurugenzi wa Ofisi ya Utafiti ya Amnesty International mjini Beirut, Lynn Maalouf tarehe 12 mwezi huu wa Julai alisema kuhusu hukumu ya kifo iliyotolewa na utawala wa Saudia dhidi ya Waislamu 4 wa madhehebu ya Shia kwamba: Utawala wa Saudia unatumia hukumu ya kifo kama silaha ya kisiasa ya kuwanyamazisha wapinzani wake. 

Panga la Aal Saudi ......

Vilevile ripoti zilizotolewa na taasisi za kutetea haki za binadamu zinasema kuwa, sababu ya asilimia 41 ya hukumu za kifo zilizotolewa na utawala wa Saudia katika mwaka huu wa 2017 ni kufanya harakati zisizokuwa za kutumia mabavu kama vile kushiriki katika maandamano ya amani ya kisaisa.  

Tags