Watu wa Yemen, wahanga wa njama za Aal Saud
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i3268-watu_wa_yemen_wahanga_wa_njama_za_aal_saud
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen amesema kuwa zinafanyika jitihada za kufikiwa mapatano ya kusitisha vita nchini humo licha ya Saudi Arabia kuzidisha mashambulizi dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 17, 2016 12:03 UTC
  • mashambulizi Yemen
    mashambulizi Yemen

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen amesema kuwa zinafanyika jitihada za kufikiwa mapatano ya kusitisha vita nchini humo licha ya Saudi Arabia kuzidisha mashambulizi dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.

Ismail Ould Sheikh Ahmed amekiri kwamba Saudia na washirika wake wamezidisha mashambulizi dhidi ya makazi ya raia nchini Yemen katika siku za hivi karibuni na kudai kuwa, zinafanyika jitihada za kupanua makubaliano ya kusitisha vita katika maeneo ya mpakani hadi katika maeneo mengine ya Yemen.

Madai hayo ya mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen yametolewa baada ya mashambulizi ya Jumanne iliyopita wakati ndege za kivita za Saudi Arabia ziliposhambulia soko lililokuwa limefurika watu na kuua raia wasiopungua 107 na kujeruhiwa wengine 90.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amelaani vikali jinai na mauaji yaliyofanywa na ndege za kivita za Saudi Arabia baada ya kushambulia soko lililokuwa limefurika watu la Khamis na kutoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka kuhusu mauaji hayo ya kutisha. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake juu ya kuendelea mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya watu wa Yemen na kusisitiza udharura wa kusitishwa machafuko na kutafutwa ufumbuzi wa mgogoro wa nchi hiyo kwa njia ya mazungumzo.

Vilevile Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa taarifa likilitaka Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuiwajibisha Saudi Arabia kutokana na ukiukaji wake mkubwa wa haki za binadamu huko Yemen. Taarifa ya Amnesty International imesema kutokana na kutojali vigezo vya keneza na kulinda haki za binadamu na kutotoa ushirikiano wa kutosha kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Saudia haipasi kuwa mwanachama katika baraza hilo.

Wakati huo huo imeripoti kuwa wanamapambano wa Yemen wameteka makumi ya vibaraka wa Saudi Arabia katika mapambano yaliyotokea kwenye mkoa al Baidaa. Jeshi na wapiganaji wa Yemen pia wameshambulia kwa makombora mjumuiko wa vibaraka wa Saudia katika mji wa al Wazaiyya na kuua idadi kadhaa miongoni mwao. Vibaraka wengine wengi wamejeruhiwa na zana zao zimeharibiwa.

Katika upande mwingine ndege za kivita za Saudi Arabia zimeendelea kushambulia maeneo mbalimbali ya Yemen ambako raia wengi wameuawa na wengine kujeruhiwa.

Katika vita vya sasa vya Yemen wapiganaji wa harakati ya Ansarullah na vikosi vya askari watiifu kwa rais wa zamani wa nchi hiyo wanapambana na waungaji mkono wa rais aliyetoroka nchi wa nchi hiyo, Abd Rabbuh Mansur Hadi anayesaidiwa na Saudi Arabia, Marekani na washirika wao. Hadi sasa maelfu ya raia wa Yemen wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi ya kila kucha ya ndege za Saudia dhidi ya makazi ya raia wa Yemen. Ndege hizo pia zimekuwa zikilenga miundo mbinu na taasisi za umma kama mahospitali, madaraja, viwanda, misikiti, shule na kadhalika.