Al Azhar yalaani mauaji ya Waislamu wa Rohingya, Myanmar
Taasisi ya Al Azhar nchini Misri imelaani vikali mauaji yanayoendelea kufanywa na Mabudha wenye misimamo mikali wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na Chuo Kikuu cha al Azhar nchini Misri imesema kuwa, mauaji hayo dhidi ya Waislamu wa Rohingya yanapingana na mafundisho ya dini zote.
Taarifa hiyo ya al Azhar imeitaka jamii ya kimataifa kukomesha mara moja mauaji ya Waislamu nchini Myanmar na kutoa wito wa kufanyika jitihada zaidi za kuzuia umwagaji damu zaidi nchini humo.
Tangu Ijumaa iliyopita Mabudha wenye misimamo mikali wamezidisha ukandamizaji na mauaji dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine na ripoti zinasema Waislamu karibu mia moja Wameuawa.
Sambamba na mauaji hayo maelfu ya Waislamu wa Rohingya wamelazimishwa kuhama nyumba na makazi yao kutokana na ukatili unaofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na jeshi la Myanmar.
Ijumaa iliyopita pia Umoja wa Mataifa ulikemea na kukosoa vikali mashambulio ya kuratibiwa ya vikosi vya usalama vya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika mkoa wa Rakhine ulioko magharibi mwa nchi hiyo.