Waislamu Warohingya Myanmar wanakabiliwa na mauaji ya kimbari
Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar wanakabiliwa na mauaji ya kimbari kwa lengo la kuwamaliza kabisa katika nchi hiyo ya bara Asia.
Hayo yamedokezwa na Masoud Shadjareh Mkuu wa Tume ya Kiislamu ya Haki za Binadamu katika mahojiano na Press TV. Ameongeza kuwa, watawala wa Myanmar wanaonekana kufanikiwa katika kuwaangamiza Waislamu huku jamii ya kimataifa ikiwa ni mwangalizi tu wa jinai hiyo. Amesema Waislamu Warohingya wanauawa kila siku katika jimbo la Rakhine magharibi mwa Myanmar.
Masoud Shadjareh amesema zinapaswa kuchukuliwa hatua za kuushurutisha Umoja wa Mataifa uwafikishe watawala wa Myanmar katika mahakama za kimataifa kufuatia jinai zao dhidi ya Waislamu. Amesema jamii ya kimataifa inapaswa kutekeleza kivitendo ile nara ya 'hatutaruhusu tena mauaji ya kimbari."
Waislamu wa Rohingya wa Myanmar zaidi ya elfu sita wameshauawa na wengine zaidi ya elfu 10 kujeruhiwa hadi sasa tangu tarehe 25 mwezi Agosti mwaka huu wakati lilipoanza wimbi jipya la mashambulizi ya ukandamizaji ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya jamii hiyo ya walio wachache katika mkoa wa Rakhine. Hadi sasa karibu Warohingya laki sita wanaripotiwa kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh kufuatia hujuma dhidi yao katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar.