Iran yataka mgogoro wa Yemen utatuliwe kidiplomasia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema kuna haja ya migogoro ya eneo, hasa mgogoro wa Yemen, kutatuliwa kwa njia za mazungumzo ya kidiplomasia.
Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter ameandia kuwa: "Huku tukikaribia mwisho wa jinamizi la Syria kupitia mazungumzo jumuishi, tunapaswa kuchukua hatua sawa na hii nchini Yemen.Haipaswi kulazimisha migogoro mipya kupitia udondoshaji mabomu, vitisho na kujiizulu. Hakuna mgogoro wowote usioweza kutatuliwa kwa njia za kidiplomasia na tumewahi kuthibitisha hilo." Zarif amesema Iran inajitahidi kuhakikisha kuwa kunapatikana amani kwa kuwajumuisha watu wote.
Saudia ilianzisha hujuma yake dhidi ya Yemen mnamo Machi mwaka 2015 kwa uungaji mkono wa Marekani kwa lengo la kuirejesha madarakani serikali kibaraka ya Abdu Rabuh Mansour Hadi aliyejiuzulu urais na kukimbilia mji mkuu wa Saudia, Riyadh.
Raia zaidi ya elfu 13 wa Yemen wameuawa, hasa wanawake na watoto, na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika uvamizi huo wa kijeshi huku Umoja wa Mataifa ukishindwa kuchukua hatua yoyote ya kuzuia jinai hizo za Saudia huko Yemen. Aidha watu zaidi ya laki sita wameambukizwa ugonjwa wa kipindupindu kote Yemen huku wengine zaidi ya 2,000 wakifarikia dunia tokea mwezi Aprili mwaka huu.