Saudia kununua mfumo wa makombora kutoka Israel
Gazeti la moja la Uswisi limefichua mpango wa Saudi Arabia kutaka kununua mfumo wa ngao ya makombora kutoka utawala wa Kizayuni wa Israel, katika hali ambayo ripoti zinasema tawala mbili hizo zipo mbioni kuimarisha uhusiano wao dhidi ya Iran.
Gazeti la Basler Zeitung linalochapishwa kwa lugha ya Kijerumani limeripoti kuwa, Saudia inataka kununua silaha kutoka Israel, ukiwemo mfumo wa ngao ya chuma ya makombora ujulikanao kama Trophy Active Protection System (APS).
Kwa mujibu wa gazeti hilo, wataalamu wa kijeshi wa Saudia tayari wameukagua mfumo huo wa kukinga makombora, katika mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abu Dhabi.
Saudia imedai kuwa inataka kununua mfumo huo kwa shabaha ya kujikinga na makombora ya balestiki yanayovurumishwa kila uchao na wanaharakati wa Ansarullah wa Yemen.
Mwaka uliopita, gazeti moja la Kizayuni lilifichua kuwa, katika mkataba wa mabilioni ya dola wa ununuzi silaha baina ya Marekani na Saudia, baadhi ya mashirika ya uundaji silaha ya Israel yalianishwa kuwa yangestafidi na makubaliano hayo.
Hivi karibuni pia afisa mmoja wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambaye hakutaka jina lake litajwe alifichua kuwa Muhammad bin Salman Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia mwezi Septemba mwaka jana alifanya safari za siri huko Israel ambapo alikutana na viongozi wa ngazi za juu wa utawala huo unaoendelea kuua watoto wa Palestina, ikiwa ni katika jitihada za kuboresha uhusiano wa Riyadh na Tel Aviv.