Kitongoji cha Trump, nembo ya ubeberu wa Marekani na Israel
Waziri wa Ujenzi wa Israel, Yoav Galant ametangaza kuwa, Tel Aviv imechukua uamuzi wa kukipa jina la "Kitongoji cha Trump" eneo kutakakojengwa balozi za nchi mbalimbali katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds.
Itakumbukwa kuwa, tarehe 6 Disemba mwaka jana, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa Washington inautambua rasmi mji wa Quds kuwa ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel. Hatua hiyo ilipingwa vikali na nchi mbalimbali dunia wakiwemo waitifaki na washirika wa Marekani yenyewe. Trump pia aliitaka Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo kutayarisha mazingira ya kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv na kwenda Quds tukufu. Wakati huo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alitangaza kuwa ubalozi wa nchi hiyo huko Quds inayokaliwa kwa mabavu utafunguliwa tarehe 14 Mei mwaka huu.
Baada ya uamuzi huo wa Trump, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliketi na kutoa uamuzi wa kutaka kufutwa uamuzi huo. Hata hivyo azimio hilo la Baraza la Usalama la UN lilipigwa kura ya veto na Marekani licha ya kupasishwa na kuungwa mkono na nchi zote 14 wanachama wa baraza hilo. Baada ya veto hiyo ya Marekani, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipeleka muswada wa azimio hilo katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambako lilipasishwa na nchi 128. Hatua hiyo iliakisi upinzani wa jamii ya kimataifa dhidi ya ubeberu na njama hiyo na Marekani na Israel dhidi ya mji mtakatifu wa Quds.
Mji wa Quds ambao una msikiti wa al Aqsa wenye kibla cha kwanza cha Waislamu ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na Palestina na ni moja kati ya maeneo matakatifu zaidi kwa Waislamu wote duniani. Hatua ya kifedhuli na iliyo kinyume cha sheria ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuamuru kuhamishiwa ubalozi wa nchi hiyo huko Quds ni sehemu ya njama kubwa ya Wazayyuni na Wamarekani dhidi ya Ulimwengu na Umma wa Kiislamu ya kutaka kulidhibiti na kuliyahudisha eneo hilo. Ni katika fremu hiyo pia ambapo Marekani inashiriki moja kwa moja katika ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.
Siku chache zilizopita redio ya Israel ilizungumzia ushirikiano mkubwa uliopo baina ya makampuni ya Marekani kama General Electric na makampuni ya Israel katika ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi huko Palestina. Vilevile hivi karibuni vyombo vya habari vilifichua kwamba jumuiya zisizo za kiserikali za Marekani zimesamehewa ushuru unaokadiriwa kufikia makumi ya mabilioni ya dola ili kushirikiana na Israel katika masuala ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi za Palestina.
Hatua hizo zote za Marekani zimeutia kiburi zaidi utawala wa Kizayuni kufanya mauaji na jinai zaidi dhidi ya Watu wa Palestina. Sera na siasa hizo za Donald Trump zinafanyika katika fremu ya siasa kuu za Marekani katika Mashariki ya Kati.