Ripoti ya kushtua kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu nchini Bahrain
Taasisi moja isiyo ya kiserikali inayotetea haki za binadamu nchini Bahrain imetoa ripoti ya kushtusha kuhusu ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini humo katika mwaka uliopita.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa jana Jumapili na Taasisi ya Haki za Binadamu ya Bahrain, utawala wa Aal Khalifa mwaka uliopita wa 2015 uliwatia mbaroni watu 1883 kwa sababu tu ya kushiriki katika maandamano dhidi ya utawala ulioko madarakani. Ripoti hiyo imeongeza kuwa vikosi vya usalama vya Bahrain viliingia ndani ya nyumba za raia wa nchi hiyo bila ya kibali katika karibu asilimia 50 ya kutiwa nguvuni watu hao. Hii ni katika hali ambayo karibu asilimia 30 ya watu hao walioko mbaroni walitiwa nguvuni wakati wakiandamana dhidi ya serikali.
Taasisi hiyo ya Haki za Binadamu isiyo ya kiserikali imeongeza kuwa, idadi halisi ya watu waliokamatwa ni kubwa zaidi kulinganisha ni ile iliyotangazwa kwa sababu familia za watu waliotiwa nguvuni zinajizuia kuwasilisha majina ya ndugu zao kwa Taasisi hiyo ya Kutetea Haki za Binadamu ili kuzuia kukamatwa tena ndugu zao. Taasisi hiyo imesema katika ripoti yake hiyo kuwa, mwaka jana wa 2015 watu wasiopungua 441 wametoweka, ambapo asilimia 38 ya watu hao ni vijana walio na umri wa chini ya miaka 18.