Wazayuni wazidi kuziyahudisha ardhi za Wapalestina
Utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea na jinai zake za kupora ardhi za Wapalestina na kuziyahudisha. Tukio la karibuni kabisa ni jinai ya utawala huo dhalimu ya kuvunja makaburi ya Wapalestina katika eneo la Jaffa lililoko umbali wa kilomita 60 kutoka Tel Aviv, mji mkuu wa utawala pandikizi wa Kizayuni.
Televisheni ya al Mayadeen imeripoti kuwa, Wazayuni wavamizi wamelivamia eneo hilo na kufukua maiti wa Waislamu na kuwatia kwenye mifuko ya plastiki ikiwa ni kukanyaga bila aibu, maadili yote ya kibinadamu. Wazayuni hao wamefanya jinai hiyo kwa madai ya kupanua eneo la shule moja ya Mayahudi.
Kabla ya hapo, Wazayuni maghasibu walivamia makaburi ya Wapalestina ya Qassam karibu na Haifa, kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kufanya unyama huo huo dhidi ya maiti wa Waislamu. Wazayuni hao walidai wamefanya jinai hiyo ya kuvunja makaburi ya Waislamu kwa ajili ya kujenga shirika moja la Israel.
Kila leo utawala wa Kizayuni unafanya njama za kuvuruga muundo wa Kiislamu wa ardhi za Palestina na kuufanya kuwa wa Kiyahudi.
Utawala huo dhalimu unaharibu kila athari ya Waislamu ikiwemo misikiti, maeneo ya kuzikiwa Waislamu, nyumba za kihistoria za Wapalestina bali kila kitu ambacho kina sura ya Kiislamu ili kwa njia hiyo ufute kikamilifu athari za Kiislamu katika maeneo unayoendelea kuwapora Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.