Utajiri wa Imarati (UAE) na Saudia unatumikia malengo ya Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i45672-utajiri_wa_imarati_(uae)_na_saudia_unatumikia_malengo_ya_wazayuni
Naibu wa Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Palestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu amesema, pesa za Imarati (UAE) na Saudi Arabia zinatumiwa kwenye mipango na njama za utawala ghasibu wa Israel kwa lengo la kununua milki za ardhi na majengo za Wapalestina kandokando ya msikiti wa Al-Aqsa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 10, 2018 16:49 UTC
  • Utajiri wa Imarati (UAE) na Saudia unatumikia malengo ya Wazayuni

Naibu wa Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Palestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu amesema, pesa za Imarati (UAE) na Saudi Arabia zinatumiwa kwenye mipango na njama za utawala ghasibu wa Israel kwa lengo la kununua milki za ardhi na majengo za Wapalestina kandokando ya msikiti wa Al-Aqsa.

Kamal Al-Khatib amesisitiza kuwa fedha za Saudi Arabia zinatumiwa kuhudumia mipango ya Marekani na Israel yenye lengo la kuifuta kadhia ya Palestina; na hatua hiyo ni uhaini na usaliti kwa watu wa mji wa Quds.

Naibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Palestina katika ardhi zilizoanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948 na kupewa jina la Israel ameashiria msaada wa dola milioni 150 zilizotolewa na Saudia kwa Idara ya Waqfu ya Quds na kubainisha kuwa fedha hizo watapatiwa watu wanaotekeleza sera mpya ya Saudi Arabia kupitia mpango uitwao "Mapatano ya Karne" na kuutangaza mpango wa Marekani na Israel katika kadhia ya Palestina.

Taswira ya mji wa Quds na msikiti mtukufu wa Al-Aqsa

Al-Khatib ameashiria pia hatua ya wafanyabiashara wa Imarati ya kununua milki za Wapalestina kandokando ya mji wa Baitul Muqaddas na kuwapatia milki hizo za ardhi na majengo walowezi wa Kizayuni na kufafanua kwamba, watu wa mji huo wa Quds wameshaung'amua mpango huo na wala hawatonasa kwenye mtego wa matapeli wa Kiimarati au wa Kiyahudi.

Nyaraka zilizofichuliwa zinaonyesha kuwa mnamo mwezi Mei mwaka 2016, Umoja wa Falme za Kiarabu, Imarati ulitekeleza mpango wa kununua milki za ardhi na majengo za eneo la kale la mji wa Baitul Muqaddas na kuziuza kwa walowezi wa Kizayuni. Mpango huo ulitekelezwa kupitia shakhsia wa Kipalestina akiwemo Muhammad Dahlan, mmoja wa viongozi wa zamani wa harakati ya Fat-h ambaye sasa ni mshauri wa Muhammad bin Zayd, mrithi wa utawala wa Abu Dhabi.../