Jun 12, 2018 13:50 UTC
  • Qatar yaishtaki Imarati katika mahakama ya haki za binadamu ya UN

Qatar imewasilisha faili la kesi dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu, katika mahakama ya juu zaidi ya Umoja wa Mataifa, ikiituhumu Abu Dhabi kwamba imekiuka haki za binadamu za wananchi wa Qatar, huku mgogoro wa nchi hizo za Kiarabu ukielekea kutimiza mwaka mmoja.

Katika kesi hiyo iliyowasilishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu ICJ yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi, Doha imeituhumu Abu Dhabi kuwa inaongoza kampeni ya ubaguzi dhidi ya Qatar, jambo ambalo linakiuka haki za binadamu za Waqatari na ambalo limekuwa na matokeo mabaya kwa wananchi wa nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.

Akizungumza juu ya kesi hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Mohammed bin Abdulrahman Aal Thani amesema, "UAE imewabagua wananchi wa Qatar kwa makusudi kwa msingi wa utaifa wao na hivyo kukiuka haki za binadamu za wananchi wa Qatar.

Uadui wa Saudia na waitifaki wake dhidi ya Qatar unaelekea kumaliza mwaka mmoja

Itakumbukwa kuwa, tarehe 23 mwezi Juni mwaka jana, Saudia, Imarati, Misri na Bahrain zilitangaza kukata uhusiano wa kidiplomasia na Qatar na kisha nchi hizo nne zikatoa masharti mazito kwa Doha. Miongoni mwa masharti hayo ni kuitaka Qatar ikate uhusiano wake wa kidiplomasia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ifunge televisheni ya al Jazeera, na ivunje uhusiano wake na makundi ya muqawama wa Kiislamu kama HAMAS ya Palestina na Hizbullah ya Lebanon.

Masharti yote hayo yamekataliwa na Qatar ikisisitiza kuwa ni kuingilia mambo yake ya ndani na haki yake ya kujitawala. 

Tags