Aug 20, 2018 14:05 UTC
  • Saudia yamkamata Imamu na Khatibu wa Masjidul Haram

Duru za habari zinasema wakuu wa Saudia wamemkamata Sheikh Saleh Aal Talib, Imamu na Khatibu wa Msikiti Mkuu wa Makka (Masjidul Haram) kutokana na hotuba aliyotoa kuhusu munkar au maovu na madhalimu.

Kwa mujibu wa gazeti la Quds al Arabi, Sheikh Aal Talib alikamatwa Jumapili na ujumbe wake wa mwisho katika ukurasa wa Twitter aliwahutubu mahujaji na pia kuweka filamu ya sehemu ya hotuba yake katika Masjidul Haram.

Wanaharakati wa kijamii wanasema hivi karibumu Sheikh Aal Talib aliandika barua ya siri iliyokosoa hali ya  mambo ya Saudia na kwamba barua hiyo pia ilimfikia mrithi wa ufalme wa Saudia Mohammad Bin Salman.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na kamatakmata ya wanazuoni na watu wanaoonekana kupinga utawala wa ukoo wa Aal Saud nchini Saudia Arabia.

Mrithi wa ufalme wa Saudia Mohammad bin Salman

Hivi majuzi wakuu wa Saudia walimkamata Sheikh Ali Bin Abar Al Zael mmoja wa mashekhe wa kabila la Shimr kutokana na ujumbe wake wa Twitter ambapo alitaka aadhibiwe mwanamfalme Abdul Azizi bin Fahd Al Saudi na kwa upande wa pili akamuombea dua mwanamfalme Nawaf bin Talal Al Rashid ambaye yuko kizuizini.

Ripoti zinasema kuwa askari usalama wa Saudi Arabia wanajiandaa kwa ajili ya kusikilizwa kesi ya vigogo wanane wa nchi hiyo waliotiwa mbaroni wakiwemo maulamaa wa kidini. 

Tags