Dec 22, 2018 02:56 UTC
  • Idadi ya wanaonyongwa Saudia imeongezkea maradufu wakati wa Bin Salman

Idadi ya watu wanaonyongwa nchini Saudi Arabia imeongezeka maradufu tokea Mohammad bin Salman ateuliwe kuwa mrithi wa kiti cha ufalme nchini humo.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, tokea Januari hadi Marchi 2018, watu 133 walinyongwa Saudi Arabia katika hali ambayo miezi minane kabla ya Bin Salman kupewa cheo cha urithi wa ufalme, idadi hiyo ilikuwa ni 67.

Gazeti hilo limeandika kuwa, tokea mwaka 2014 hadi hivi sasa watu karibu 700 wamenyongwa Saudi Arabia. Ripoti hiyo imeongeza kuwa, miongoni mwa walionyongwa ni raia wa kigeni ambao inadaiwa walihusika na biashara ya mihadarati.

Saudi Arabia imekuwa ikiwanyonga wapinzani wa utawala wa kifalme kwa visingizio mbali mbali na sasa unyongaji huo unawalenga pia raia wa kigeni ambao wengi wao wananyongwa kiholela.

 Jamal Khashoggi

Kwa mujibu wa ripoti za Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia, kuanzia mwaka 2011 hadi 2018, Waindonesia 103 wamenyongwa Saudia na aghalabu walikuwa ni wafanyakazi wa ndani ya nyumba. Waindonesia hao wamenyongwa kwa visingizio visivyo na msingi na wamenyongwa pasina kuwepo mahakama adilifu ya kusikiliza kesi zao.

Aidha hivi karibuni Shirika la Human Rights Watch la kutetea haki za binadamu limetoa taarifa na kutaka Saudia isitishe  unyongaji wa kinyama nchini humo.

Ukatili wa Saudia pia umevuka mipaka ya nchi hiyo ambapo Jamal Khashoggi, aliyewahi kuwa msiri na mwandani wa aila ya kifalme inayotawala nchini Saudi Arabia, lakini hatimaye akageuka kuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal Saud, aliuliwa kikatili na mwili wake kukatwa vipande vipande, alipoingia kwenye jengo la ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki mnamo tarehe Pili Oktoba ili kukabidhi hati zake kwa ajili ya mpango wake wa kufunga ndoa. Katika faili la sauti lililorekodiwa wakati wa ukatili huo, ilisikika sauti ya msumeno ukikeketa na kuukata vipande vipande mwili wa mwandishi huyo.

Tags