Daesh: Ikhwanul Muslimin ya Misri ni makafiri na mamurtadi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i5041-daesh_ikhwanul_muslimin_ya_misri_ni_makafiri_na_mamurtadi
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limeitaja harakati kuu ya Waislamu wa Kisunni nchini Misri ya Ikhwanul Muslimin kuwa ni kundi la makafiri walioritadi na kuuasi Uislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 14, 2016 09:54 UTC
  • Daesh: Ikhwanul Muslimin ya Misri ni makafiri na mamurtadi

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limeitaja harakati kuu ya Waislamu wa Kisunni nchini Misri ya Ikhwanul Muslimin kuwa ni kundi la makafiri walioritadi na kuuasi Uislamu.

Katika makala ya kurasa 25 iliyochapishwa katika jarida lao la kipropaganda la Dabiq, kundi hilo la kitakfiri limesema kuwa limeitaja Ikhwanul Muslimin kama harakati ya kikafiri kwa kuwa inashirikiana na harakati ya Kiislamu ya Palestina Hamas sambamba na kuunga mkono kubuniwa kwa taasisi za kidemokrasia. Kadhalika kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limeituhumu Ikhwani kuwa inapanga njama ya kuzusha vita dhidi ya Uislamu na Waislamu. Makala hiyo imekashifu hatua ya Ikhwani kutokana na kile ilichokitaja kuwa, kuunga mkono demokrasia kwa kuwa na wabunge katika bunge la Misri; huku ikiitaja demokrasia kuwa mfumo wa kikafiri unaotukuza na kuwapa wanadamu cheo kuu.

Hii ni katika hali ambayo, maelfu ya wapinzani na wanachama wa ngazi za juu wa Ikhwanul Muslimin wametiwa mbaroni na mamia ya wengine kuuliwa huko Misri, kutokana na juhudi zao za kurejesha uhuru na izza katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Mohammed Badie, Kiongozi wa Ikhwanul Muslimin anashikiliwa katika korokoro ya Misri kwa zaidi ya miaka miwili sasa, akituhumiwa kwa makosa mbalimbali na hadi kufikia sasa amekatiwa hukumu mbili, moja ikiwa ni ya kunyongwa na nyingine ya kifungo cha maisha jela.