Chama tawala cha Baath chashinda viti vingi uchaguzi wa bunge Syria
-
Uchaguzi Syria
Chama tawala cha Baath kimeshinda aghalabu ya viti katika uchaguzi wa bunge uliofanyika nchini Syria hivi karibuni.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Syria imesema kuwa, chama hicho cha Rais Bashar al-Assad ambacho kilikuwa chini ya muungano wa Umoja wa Taifa kimeshinda viti 200 kati ya 250 vya bunge la nchi hiyo. Zaidi ya wagombea 11,300 walikuwa wametangaza azma yao ya kuwania viti hivyo lakini 3,500 pekee ndiyo waliosalia katika kinyang'anyiro hicho kwenye uchaguzi wa Aprili 13. Hisham al-Shaar, Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Syria amesema kuwa, kati ya wapiga kura zaidi ya milioni 8 na laki 8 waliosajiliwa, zaidi ya milioni 5 wameshiriki zoezi hilo la kuainisha mustakabali wa nchi hiyo. Rais Bashar al-Assad amekuwa akisisitiza kuwa, mgogoro wa Syria utatatuliwa na wananchi wenyewe na kwamba uchaguzi huo wa bunge ni moja ya mikakati ya kuupatia ufumbuzi mzozo huo. Kadhalika Rais Assad ameonya kuwa, mpango wowote wa kuifanya Syria iwe chini ya mfumo wa Shirikisho hautakuwa na tija kwa taifa hilo. Kwa muda mrefu sasa serikali ya Syria imekuwa ikisisitiza kuwa magaidi nchini humo wanapata misaada ya fedha na silaha kutoka nchi za Magharibi hasa Marekani na waitifaki wake katika eneo hili ambao ni Saudi Arabia, Qatar, Uturuki na utawala haramu wa Israel. Karibu watu nusu milioni wameshapoteza maisha tokea magaidi waanzishe kampeni ya kumuondoa madarakani Rais Bashar al Assad wa Syria mwaka 2011.