Hizbullah: Saudia inagharamia jinai za Marekani na Israel Asia Magharibi
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon (Hizbullah) ameitaja Saudi Arabia kama mzizi wa ukosefu wa uthabiti katika eneo la Asia Magharibi, na kwamba utawala huo wa kifalme ndio unaofadhili na kugharamia jinai zinazofanywa na Marekani na utawala haramu wa Israel katika eneo.
Sheikh Naim Qassim aliyasema hayo jana jioni wakati akihutubu katika marasimu yaliyofanyika katika mji wa Kfar Fila, kusini mwa Lebanon na kubainisha kuwa, ni jambo la kusikitisha namna Riyadh inavyogharamia jinai hizo za Marekani kwa kutumia fedha za wananchi maskini wa nchi hiyo.
Amesisitiza kuwa, utawala wa Aal-Saud umeibadilisha Saudia kuwa utawala wa maovu.
Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, utawala wa Riyadh ni mfano hai wa utawala wa kidhalimu na kidikteta, unaoshinikizwa na Marekani kufanya kila aina ya ovu, kwa shabaha ya kuufanya wa kawaida uhusiano kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sheikh Naim Qassim ameeleza bayana kuwa, Marekani inafanya juhudi za kuanzisha Asia Magharibi Mpya ambayo Washington itakuwa na udhibiti wa kila kitu na kwa msingi huo kusiweko na nchi mingoni mwa nchi za eneo hili yenye nguvu na mamlaka ya kujitawala na kujiamulia mambo yake, lakini katu wananchi wa eneo hili hawatasalimu amri na muqawama utaendelea.
Kadhalika Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameashiria kitendo cha utawala wa Aal-Saud cha kutekeleza hukumu ya kuwanyonga makumi ya Waislamu wa Kishia nchini humo, ambapo amebainisha kuwa, ilichofanya Saudia ni mauaji ya halaiki kwa kutumia kisingizio cha kupambana na ugaidi kuwanyonga kwa umati wanaharakati, wanazuoni na wakosoaji wake.