Hizbullah ya Lebanon: Marekani haithubutu kuanzisha vita dhidi ya Iran
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa vitisho vya Marekani dhidi ya Iran na kulegeza msimamo Trump mbele ya Tehran ni mambo yanayoonesha kuwa Washington haina uthubutu wa kuanzisha vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Sheikh Naim Qassim alisema hayo jana katika mahojiano na shirika la habari la IRNA na huku akigusia uwezo wa kambi ya muqawama wa kuzuia mashambulizi katika eneo hili ameongeza kuwa, kamwe Tehran haitakuwa ya kwanza kuanzisha vita na kwamba msimamo wa Iran ni wa kujihami mbele ya vitisho vya kijeshi vya Trump na kulegeza kwake msimamo kuhusu vitisho vyake hivyo.
Baada ya kupanda joto la wasiwasi wa kutokea vita katika eneo la Mashariki ya Kati kutokana na vitisho vya Marekani dhidi ya Iran, hatimaye rais wa Marekani amebadilisha msimamo na kudai kuwa Washington haina nia ya kuingia vitani na Iran wala haitaki kuupindua mfumo wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu, bali kitu pekee inachotaka ni kuhakikisha kuwa Iran haina "silaha za nyuklia."
Jumapili iliyopita pia Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alilegeza msimamo sana kuhusu masharti 12 yaliyowekwa na nchi yake kuhusu Iran na kudai kuwa White House iko tayari kufanya mazungumzo na Iran bila ya masharti yoyote.
Sheikh Naim Qassim amezungumzia pia jinai za utawala wa Kizayuni za kuendelea kuingia bila ya ruhusa katika mipaka ya angani na majini ya Lebanon na kusisitiza kuwa, kwa mara chungu nzima Lebanon imekuwa ikiulalamikia Umoja wa Mataifa na kuutaka uchukue hatua za kuulazimisha utawala wa Kizayuni ukomeshe jinai zake hizo dhidi ya Lebanon.