Kushtadi lawama na ukosoaji kwa uhusiano wa Marekani na Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i5446-kushtadi_lawama_na_ukosoaji_kwa_uhusiano_wa_marekani_na_saudia
Rais Barack Obama wa Marekani anaelekea Saudi Arabia leo kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo huku lawama na ukosoaji ukiwa umeshtadi kwa uhusiano baina ya Washington na Riyadh.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 20, 2016 03:22 UTC
  • Kushtadi lawama na ukosoaji kwa uhusiano wa Marekani na Saudia

Rais Barack Obama wa Marekani anaelekea Saudi Arabia leo kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo huku lawama na ukosoaji ukiwa umeshtadi kwa uhusiano baina ya Washington na Riyadh.

Katika safari yake hiyo, Obama anafuatana na msemaji wa White House Josh Earnest, pamoja na Mshauri wa Usalama wa Taifa Susan Rice. Leo Rais wa Marekani anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Mfalme Salman wa Saudia kuhusu kupambana na makundi ya kitakfiri, mgogoro wa Syria, vita vya Yemen pamoja na maudhui nyenginezo ikiwemo hitilafu baina ya Saudia na Iran na pia uwezekano wa kuhusika utawala wa Aal Saud katika mashambulio ya Septemba 11, mwaka 2001 nchini Marekani.

Kesho Alhamisi, Obama anatazamiwa kushiriki katika kikao cha pamoja na viongozi wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (P)GCC linalozijumuisha Saudi Arabia, Kuwait, Umoja wa Falme za Kiarabu, Oman, Bahrain na Qatar.

Hayo yanajiri wakati hivi sasa kuna masuala kadhaa ambayo yamezusha hitilafu baina ya Washington na Riyadh, muhimu zaidi ukiwa ni mpango wa Kongresi ya Marekani unaotoa fursa kwa raia wa nchi hiyo kuwashtaki viongozi na utawala wa Saudia kwa kuhusika katika matukio ya Septemba 11.

Pamoja na hayo Paul Ryan, Spika wa Kongresi ya Marekani alitangaza siku ya Jumanne mara baada ya kikao na wajumbe wa chama chake cha Republican katika baraza hilo, kuwa Kongresi inapaswa kuangalia upya uamuzi wa kupitisha sheria ya kuifuatilia kisheria serikali ya Saudi Arabia kuhusiana na mashambulio ya Septemba 11, sheria ambayo itawaruhusu raia wa Marekani kufungua mashtaka dhidi ya utawala wa Riyadh.

Ryan aliongezea kwa kusema:"kwa mtazamo wangu tunapaswa kuangalia tena uamuzi wa kupitisha sheria kama hii ambayo itaupa changamoto uhusiano wetu na Wasaudi."

Toleo la Ijumaa iliyopita la gazeti la New York Times liliandika kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Adel al-Jubeir aliwataarifu wajumbe wa Kongresi ya Marekani kwamba endapo rasimu ya sheria hiyo itapasishwa nchi yake italazimika kuzihamisha nchini humo mali zake zenye thamani ya dola bilioni 750.

Kevin Barret, mwandishi na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Madison amesema kuhusiana na kadhia hiyo kwamba serikali ya Marekani haiziweki hadharani nyaraka za matukio ya Septemba 11 na kwamba ufichaji wake huo wa mambo unazuia kufichuka ukweli kuhusu matukio hayo. Barret amefafanua kuwa kuna ripoti ya siri ya kurasa 28 iliyopunguzwa baadhi ya taarifa zake ambayo imetayarishwa kuhusiana na matukio ya Septemba 11 ikionyesha jinsi Saudia ilivyohusika katika matukio hayo.

Hii ni katika hali ambayo, ndani ya Marekani kwenyewe zimetolewa lawama kali kuhusu nafasi ya Saudi Arabia katika uundaji makundi ya kigaidi. Ben Rhodes, Naibu Mshauri wa Usalama wa Taifa amekiri kuwa Saudia ilihusika katika uundaji wa kundi la kigaidi la al-Qaeda.

Amesema kundi la kigaidi la al-Qaeda liliundwa na kuratibiwa kwa pesa za Saudia na akaeleza bayana kuwa siasa na sera hizo za utawala wa Riyadh hazijaishia kwa al-Qaeda bali kuna baadhi ya matajiri wa Saudia ambao wanayasaidia makundi yenye kufurutu mpaka ambapo baadhi ya wakati misaada hiyo hutolewa moja kwa moja kwa makundi hayo.

Rey Takeyh, afisa wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Nje na mjumbe mwandamizi wa Baraza la Uhusiano wa Nje la nchi hiyo ameashiria hitilafu kadha wa kadha zilizopo baina ya Washington na Riyadh na kueleza kwamba safari ya sasa ya Barack Obama huko Saudi Arabia ndio "safari yake ya mwisho" na yamkini "isiyo na faida zaidi" wakati akiwa Rais wa Marekani. Takeyh vilevile amesisitiza kuwa kutokana na mabadiliko yaliyojitokeza katika soko la nishati duniani, leo Marekani haitegemei tena mafuta ya Saudia, na kwamba utegemezi na uhitaji wa mafuta hayo haupo tena.../