Omar Sahabou: Imarati ina woga wa wimbi la demokrasia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54598-omar_sahabou_imarati_ina_woga_wa_wimbi_la_demokrasia
Mwanasiasa mashuhuri wa Tunisia kutoka chama cha Nidaa Tunis amesema kuwa serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu ina woga wa kupenya demokrasia na kuingia nchini humo; kwa sababu hiyo inafanya jitihada za kuangamiza demokrasia nchini Tunisia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 06, 2019 21:53 UTC
  • Omar Sahabou: Imarati ina woga wa wimbi la demokrasia

Mwanasiasa mashuhuri wa Tunisia kutoka chama cha Nidaa Tunis amesema kuwa serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu ina woga wa kupenya demokrasia na kuingia nchini humo; kwa sababu hiyo inafanya jitihada za kuangamiza demokrasia nchini Tunisia.

Omar Sahabou ambaye ni miongoni mwa waasisi wa chama cha Nidaa Tounes amesema Imarati inatumia mbinu zote zinazowezekana kwa ajili ya kuua demokrasia nchini Tunisia kwa sababu ina woga wa kupenya kile inachokiita kuwa ni "maradhi au kirusi cha demokrasia" na kuingia nchini humo.  

Sahabou ameongeza kuwa, afisa mmoja wa Imarati alimwambia waziwazi kwamba, Waimarati wana maisha mazuri na ya ukwasi lakini wana tatizo moja kubwa ambalo ni Tunisia.

Mwanasiasa huyo wa Tunisia amesema: "Waimarati wanataka kuua mfumo wa demokrasia ya Tunisia kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwatesa Watunisia kwa njaa, kueneza ufuska na mashambulizi ya kigaidi, na inasikitisha kuona kwamba, baadhi ya makundi yenye misimamo mikali ndani ya nchi yana malengo hayo hayo ya kuiondoa madarakani serikali ya kidemokrasia." 

Watawala wa Imarati

Mwaka jana mtandao wa Mondafrique wa Ufaransa unaofuatilia masuala ya Afrika ulivinukuu vyombo vya kidiplomasia kwamba, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia aliyeuzuliwa, Lotfi Braham alikutana kwa siri na mkuu wa shirika la ujasusi la Imarati katika kisiwa cha Djerba na kupanga njama ya kufanya mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Beji Caid Essebsi wa nchi hiyo.

Mtandao huo ulifichua kwamba, mkutano huo ulifanyika baada ya mkuu wa shirika la ujasusi la Imarati kurejea nchini kwake baada ya kushiriki katika kikao cha Paris kilichotayarishwa na Rais Emmanuel Macron kuhusu Libya 29 mwezi Mey 2018.