Ripoti: Imarati imeondoa askari wake Yemen kwa sababu Saudia haitashinda vita
Ripoti iliyofichuliwa hivi karibuni imebaini kuwa Imarati ambayo ni mshirika muhimu katika muungano wa vita vya Saudi Arabia nchini Yemen imeamua kuondoa majeshi yake nchini humo kwa sababu ni muhali kuweza kushinda vita hivyo.
Waraka uliofichuliwa kwa waandishi habari unaeleza kuwa, Imarati imefikia natija kwamba muungano wa Saudia huko Yemen hauwezi kushinda vita na kwamba hiyo ndiyo sababu kuondoa majeshi yake huko Yemen.
Yapata mwezi mmoja uliopita Imarati ilitangaza kuwa imenza kuwaondoa wanajeshi wake nchini Yemen ambako wanashiriki katika muungano wa vita unaoongozwa na utawala wa kifalme wa Saudi Arabia dhidi ya taifa la Yemen kwa kipindi cha miaka minne sasa.
Awali Abu Dhabi ilikuwa imetangaza sababu mbalimbali za kuondoa majeshi yake nchini Yemen ikiwa ni pamoja na wasiwasi kuhusu usalama wake wa ndani au kwamba ni mbinu tu ya kijeshi kwa ajili ya kujipanga upya au kwamba inawaondoa askari hao nchini Yemen ili kuunga mkono mpango wa amani wa Umoja wa Mataifa.
Uamuzi huo wa Imarati ambayo sambamba na Marekani, Israel na Uingereza ni mshirika muhimu katika vita vya Saudia Arabia nchini Yemen, umewakasirisha sana watawala wa Riyadh. Saudia imekuwa ikiitegemea sana Imarati katika vita vya Yemen kutokana na kutumia askari na wapiganaji mamluki kutoka maeneo mbalimbali.
Wachambuzi wa mambo wanasema mashambulizi ya jeshi la Yemen na wapiganaji wa harakati ya Ansarullah dhidi ya viwanja vya ndege na meli za kivita za Saudia na waitifaki wake na ilevile mauaji ya idadi kubwa ya askari wa Saudia na Imarati huko Yemen imeilazimisha Abu Dhabi kutazama upya nafasi yake katika vita vya Yemen.