Wanamgambo wa Saudia na Imarati wazidi kutwangana nchini Yemen
Baada ya wanamgambo wanaofadhiliwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kuimarisha nguvu zao na kuudhibiti mkoa wa Aden hasa baada ya ndege za kivita za Imarati kuwashambulia wanamgambo wanaoungwa mkono na Saudi Arabia, ugomvi baina ya wavamizi wa Yemen umezidi kuonekana.
Mtandao wa habari wa "al Khaleej Online" umeripoti habari hiyo leo Jumamosi na kuongeza kuwa, hatua ya Imarati ya kuwashambulia kwa ndege askari wa Mansour Hadi wanaoungwa mkono kifedha na kijeshi na Saudia kunathibitisha kuwa malengo ya Umoja wa Falme za Kiarabu yanakinzana na yale ya Saudia nchini Yemen.
Watawala wa Imarati wanawaunga mkono wanamgambo wanaotaka kujitenga maeneo ya kusini mwa Yemen. Katika taarifa yake ya kwanza rasmi, viongozi wa Saudi Arabia wamewataka viongozi wa Imarati waache kuwasaidia wanamgambo wanaopigania kujitenga. Ingawa mwito huo umetolewa kwa njia isiyo ya moja kwa moja, lakini viongozi wa Riyadh wamelaani mashambulizi dhidi ya askari wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Abdu Rabbuh Mansour Hadi wanaojulikana kwa jina la Baraza la Mpito la Kusini mwa Yemen wanaoungwa mkono na Imarati.
Katika siku za hivi karibuni, mitandao ya kijamii imekuwa ikifichua waziwazi ugomvi uliopo baina ya wavamizi wa Yemen, yaani Saudi Arabia na Imarati huku kila mmoja akimtuhumu mwenzake kutokana na hali iliyojitokeza hivi sasa.
Nchi hizo mbili zilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya nchi maskini ya Yemen mwezi Machi 2015 kwa tamaa kwamba zingeliweza kuiteka nchi hiyo nzima katika kipindi kifupi tu. Hata hivyo hivi sasa tumo kwenye mwaka wa tano wa tangu kuanza uvamizi huo na kila leo wavamizi wa Yemen wanazidi kupata pigo kutoka kwa wanamapambano wenye uchungu na nchi yao ya Yemen.