Marekani kutuma wanajeshi zaidi huko Saudia na Imarati
Marekani inajiandaa kutuma askari zaidi nchini Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, kuimarisha kile kilichotajwa kama mfumo wa ulinzi wa anga wa Riyadh.
Mpango huo umeaidhinishwa na Rais Donald Trump, kufuatia maombi ya Saudia na Imarati.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Mark Esper amedai kuwa, "Katika kujibu ombi la utawala wa kifalme, rais ameidhinisha kutumwa vikosi zaidi, ambavyo vitajikita zaidi katika kuimarisha ulinzi wa anga na mifumo ya makombora."
Amesema Pentagon inafanya juu chini kuharakisha mchakato wa kutuma zana za kijeshi huko Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu ili kuimarisha uwezo wao wa kujilinda.
Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya jeshi la Yemen kwa kushirikiana na kamati za wananchi za nchi hiyo na katika kujibu hujuma na mashambulizi ya Saudia na pia mzingiro wa kila upande wa muungano vamizi dhidi ya taifa hilo masikini (Yemen), lilivishambulia vituo vya kusafishia mafuta vya Buqayq na Khurais vya Saudia .
Kutokana na shambulizi hilo la Jumamosi iliyopita, shughuli za uzalishaji mafuta za Riyadh zilisimama kwa muda, na hivyo kupelekea bei ya mafuta katika soko la dunia kupand sambamba na kuporomoka kwa soko la hisa nchini humo kwa zaidi ya asilimia 2.