Marekani kutuma silaha na maelfu ya askari wake nchini Saudia
Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imesema inajiandaa kutuma wanajeshi wake 3000 nchini Saudi Arabia.
Msemaji wa Pentagon, Jonathan Hoffman amesema Mark Esper, Waziri wa Ulinzi wa Marekani tayari ameidhinisha mpango huo wa kutumwa wanajeshi zaidi wa Marekani nchini Saudia.
Amesema mbali na waelfu ya wanajeshi, Washington itatuma pia nchini Saudia mfumo wa kujilinda na mashambulizi ya makombora (THAAD), manowari mbili za kijeshi na ndege za kivita miongoni mwa silaha nyinginezo.
Mapema jana, Mark Esper, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alizungumza kwa njia ya simu na Mrithi wa Ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman na kumueleza kuwa kutumwa kwa wanajeshi na silaha hizo za Marekani ni kwa lengo la kuimarisha uwezo wa kujilinda wa Saudi Arabia.
Jana Ijumaa akizungumza kwa dharau na majivuno, Rais Donald Trump wa Marekani alisema "Washington inatuma askari zaidi nchini Saudi Arabia ili kuwasaidia Wasaudia. Riyadh imekubali kugharamia kila kitu tunachowafanyia."
Haya yanajiri chini ya mwezi mmoja baada ya jeshi la Yemen kwa kushirikiana na kamati za wananchi za nchi hiyo na katika kujibu hujuma na mashambulizi ya Saudia na pia mzingiro wa kila upande wa muungano vamizi dhidi ya taifa hilo masikini (Yemen), kuvishambulia vituo vya kusafishia mafuta vya Buqayq na Khurais vya Saudia licha ya uwepo wa askari na mifumo na zana za kijeshi za Marekani nchini humo.
Kutokana na shambulizi hilo la Septemba 15, shughuli za uzalishaji mafuta za Riyadh zilisimama kwa muda, na hivyo kupelekea bei ya mafuta katika soko la dunia kupanda. Shambulio hilo liliisababishia Riyadh hasara ya zaidi ya dola bilioni 2.