Apr 24, 2016 04:32 UTC
  • Watu 12 wauawa katika  hujuma za kigaidi mjini Baghdad, Iraq

Kwa akali watu 12 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mashambulizi mawili ya bomu katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Habari zinasema kuwa, shambulizi la kwanza lilifanyika karibu na kituo cha upekuzi katika eneo la Husseiniya kaskazini mwa mji huo na kuua watu tisa na kujeruhi wengine 28.

Shambulizi la pili lililenga msafara wa magari ya kijeshi katika eneo la Arab Jabour, kusini mashariki mwa mji mkuu wa Baghdad na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine 11 kujeruhiwa.

Hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na miripuko hiyo ya mabomu ya kutegwa garini jana jioni, lakini aghalabu ya hujuma za aina hii zimekuwa zikifanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.

Ijumaa iliyopita, watu wasiopungua tisa waliuawa na wengine zaidi ya 25 kujeruhiwa baada ya bomu kulipuka ndani ya msikiti mmoja katika eneo la Radwaniyah kusini magharibi mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Aidha siku ya Alkhamisi kulijiri miripuko mingine katika maeneo kadhaa ya mji wa Baghdad ambapo watu wanane waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Idara ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq inasema Wairaqi 1,119 waliuawa kote Iraq katika hujuma za kigaidi mwezi uliopita wa Machi pekee.

Tags