Saudia yaendelea kushikilia rekodi ya kuwa mnunuzi mkuu wa silaha duniani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i59653-saudia_yaendelea_kushikilia_rekodi_ya_kuwa_mnunuzi_mkuu_wa_silaha_duniani
Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) imetangaza kuwa, Saudi Arabia ndiyo nchi inayoongoza kwa ununuaji silaha duniani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 10, 2020 04:45 UTC
  • Saudia yaendelea kushikilia rekodi ya kuwa mnunuzi mkuu wa silaha duniani

Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) imetangaza kuwa, Saudi Arabia ndiyo nchi inayoongoza kwa ununuaji silaha duniani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Ripoti ya taasisi hiyo ya kimataifa iliyotolewa jana Jumatatu inaonyesha kuwa, ununuaji silaha na zana za kijeshi unaofanywa na Saudi Arabia hususan kutoka Marekani umeongezeka kwa asilimia 130 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka jana 2019.

Taasisi ya SIPRI imebainisha katika ripoti yake hiyo kuwa, Marekani na Uingereza zimeendelea kuziuzia Saudia ndege za kivita, magari ya deraya pamoja na zana zingine za kijeshi kwa ajili ya kutumia katika vita vilivyoanzishwa na utawala wa Riyadh dhidi ya Yemen.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 73 ya silaha ilizonunua Saudia katika kipindi hicho cha miaka mitano ni kutoka Marekani, huku asilimia 13 ya silaha hizo zikitoka Uingereza.

Marekani, muuzaji mkubwa wa silaha duniani

Ripoti hiyo ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm imefichua kuwa, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nazo pia ni miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza kwa ununuzi wa silaha duniani.

SIPRI imesema kiwango cha usafirishaji nje silaha duniani kimeongezeka kwa asilimia 12 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, huku Marekani ikiongoza kwa kusafirisha nje silaha.