Harakati ya Hizbullah: Njama za Marekani hazitopunguza muqawama wa Wairaki
-
Abu Israel, Mmoja wa makomando shupavu wa Harakati ya Hizbullah ya Iraq, aliyeweza kuangamiza idadi kubwa ya magaidi wa Daesh (ISIS)
Harakati ya Hizbullah ya Iraq imesema kuwa, hatua chafu za Marekani dhidi ya nchi hiyo, hazitakuwa na taathira yoyote kwenye muqawama wa Wairaki.
Hii ni baada ya gazeti la New York Times la nchini Marekani kuandika kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imewatumia barua ya siri makamanda wake wa kijeshi ikiwataka waandae mpango wa kuzidisha harakati zao za kijeshi nchini Iraq na kufanya juhudi za kuifuta Harakati ya Hizbullah nchini humo. Kufuatia taarifa hiyo Harakati hiyo ya Hizbullah imetoa taarifa ikibainisha kuwa, njama zote za kutwishwa zinazotekelezwa na Marekani dhidi ya muqawama wa Iraq zitaishia kufeli.
Aidha harakati hiyo sambamba na kuashiria vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran imeongeza kuwa, hivi sasa ulimwengu umechoka na hatua za Washington ambazo hazina lengo jingine ghairi ya kuchochea vita, ugaidi na njama dhidi ya mataifa. Itakumbukwa kuwa Alkhamisi iliyopita Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza kuwawekea vikwazo watu 15 na asasi tano zenye mfungamano na Iran na kudai kuwa vikwazo hivyo ni kwa ajili ya kukabiliana na ugaidi. Hii ni katika hali ambayo katika wiki za hivi karibuni na kufuatia kuenea virusi vya Corona katika nchi tofauti za dunia ikiwemo pia Iran, asasi mbalimbali za kimataifa na viongozi wa nchi tofauti za dunia wakiwemo wa Uturuki, Russia, Pakistan na China wameitaka Washington kufuta vikwazo vyake vya upande mmoja na vilivyo kinyume cha sheria dhidi ya Iran.