Yemen yakaribia kutumbukia kwenye mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60733-yemen_yakaribia_kutumbukia_kwenye_mgogoro_mbaya_zaidi_wa_kibinadamu
Vita dhidi ya Yemen vimepelekea mamilioni ya watu wa nchi hiyo kuwa wakimbizi na wanawake pamoja na watoto kukabiliwa na magonjwa na mgogoro mkubwa wa baa la njaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 02, 2020 05:46 UTC
  • Yemen yakaribia kutumbukia kwenye mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu

Vita dhidi ya Yemen vimepelekea mamilioni ya watu wa nchi hiyo kuwa wakimbizi na wanawake pamoja na watoto kukabiliwa na magonjwa na mgogoro mkubwa wa baa la njaa.

Huku akisema siku ya Ijumaa kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba jinai za Wasaudi na kuenea virusi vya Covid-19 nchini Yemen kumeisukuma nchi hiyo kwenye ukingo wa mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu, Abbas Musawi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Kwa kupata faida kubwa inayotokana na mauzo ya silaha kwa Saudia, mikono ya serikali ya Uingereza imejaa damu ya watu wa Yemen wasio na hatia. Ameongeza kwa kusema: Uingereza inapasa kuwa katika upande mzuri wa historia.

Hata kama Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza anajaribu kuonyesha kuwa ni miongoi mwa watu wanaotaka kuhitimishwa vita vya Yemen lakini kama inavyoonyesha ripoti ya shirika la kimataifa la Oxfam; tokea mwezi Januari mwaka 2015 hadi sasa, Uingereza imetoa kibali cha kuuziwa Saudi Arabia silaha zenye thamani ya pauni bilioni 604 na ina nafasi muhimu katika kutoa mafunzo kwa askari wa nchi hiyo ya Kiarabu. Nukta muhimu inayoashiriwa katika ripoti hiyo ya Oxfam ni kuwa mauazo ya silaha hizo yameongezeka hasa baada ya kutiwa saini Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Silaha ATT ulioanza kutekelezwa tarehe 24 Disemba mwaka 2014.

Abbas Musawi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Mkataba huo ambao ni wa pande kadhaa unalenga kuratibu biashara ya kimataifa ya silaha za kawaida ili kufikiwa amani ya kieneo na kimataifa, kupunguza machungu ya wanadamu, kuimarisha ushirikiano na kuwepo uwazi na uwajibikaji wa viongozi ndani ya nchi na baina ya nchi tofauti.

Andrew Smith, Msemaji wa Kampeni ya Uingereza Dhidi ya Biashara ya Silaha CAAT ametoa radiamali kuhusiana na ripoti hiyo ya Oxfam kwa kusema: Hapana shaka kwamba silaha za Uingereza zimekuwa na nafasi haribifu nchini Yemen. Ndege za kivita za Uingereza huwa zinapaa katika anga ya Yemen na kuwadondoshea vichwani watu wa Yemen mabomu na makombora yaliyotengenezwa katika nchi hii.

Mwaka 2015, Saudi Arabia na Imarati zilianzisha muungano wa kijeshi wa nchi kadhaa za Kiarabu na kwa ushirikiano wa karibu wa Marekani zikaivamia Yemen, ambayo ni nchi masikini zaidi ya Kiarabu, kwa kisingizio cha kumrejesha madarakani Abdurabbuh Mansur Hadi, rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuikimbia nchi, ili tu ziweze kufikia malengo yao ya kisiasa katika nchi hiyo.

Hii leo tunashuhudia masuala mawili muhimu huko Yemen. La kwanza ni kuwa biashara ya silaha bado inaendelea licha ya kusababisha maafa ya kinbinadamu nchini humo. Suala la pili ni kuwa jinai za kibinadamu zinazotekelezwa katika nchi hiyo zinatokana na biashara hiyo ya silaha.

Wanaharakati wa kampeni ya CAAT

Vita vya Yemen vimepelekea kuharibiwa shule, hospitali na miuondombinu mingine muhimu katika nchi hiyo. Silaha hizo zinazouzwa na nchi za Magharibi kwa vibaraka wao wa Kiarabu hadi sasa zimepelekea maelfu ya Wayemen wasio na hatia kuuawa kinyama na wengine wanaokaribia milioni kumi kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi yao. Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, janga la njaa katika nchi hiyo limebadilika na kuwa maafa makubwa zaidi ya kibinadamu duniani.

Kwa msingi huo ni wazi kuwa vita hivyo haviwezi kumalizika bila ya kukomeshwa mauzo ya silaha kwa wavamizi. Maandishi ya Twitter ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kuhusu Uingereza yana ujumbe wa wazi na wa moja kwa moja katika uwanja huo.