Muungano wa kivita wa Saudia watekeleza hujuma 450 dhidi ya Yemen
Muungano wa kivita wa Saudi Arabia umetekeleza mashambulizi 450 ya anga dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Yemen katika kipindi cha wiki moja iliyopita.
Katika taarifa, Msemaji wa Majeshi ya Yemen Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema katika kipindi cha wiki moja iliyopita, ndege za kivita za Saudi Arabia zimetekeleza mashambulizi 450 dhidi ya maeneo ya raia katika mikoa ya Maarib, Al Jouf, Sanaa, Amran, Saada, Hajjah na Al Baidhaa.
Wakati huo huo, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, limejiunga na mashirika mengine ya haki za binadamu katika kukemea na kukosoa uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kufuta jina la Saudi Arabia na washirika wake katika vita vya Yemen kwenye orodha nyeusi ya nchi zinazoua watoto na kuvunja haki zao.
Ripoti ya Amnesty International imesema kuwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameliondoa jina la muungano wa vita huko Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia katika orodha nyeusi ya wauaji wa watoto huku akijua kwamba athari mbaya na haribifu za vita vya Yemen zitaendelea kuvitesa vizazi vijavyo.
Guterres alichukua uamuzi huo wiki iliyopita siku chache baada ya Kituo cha Haki za Binadamu cha Ainul Insaniya kutoa ripoti na kutangaza kuwa, tokea muungano wa Saudia uanzishe vita dhidi ya Yemen mnamo Machi 26, 2015 hadi sasa, watu 16, 672 wamepoteza maisha na miongoni mwao kuna watoto 3,742 na wanawake 2,364.
Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.
Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani na utawala haramu wa Israel.