Vielelezo muhimu vya Uchaguzi wa Bunge nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i62324-vielelezo_muhimu_vya_uchaguzi_wa_bunge_nchini_syria
Tarehe 19 Julai, wananchi wa maeneo tofauti ya Syria walijitokeza kwenye maeneo ya kupigia kura kwa ajili ya kushiriki katika Uchaguzi wa Bunge.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 21, 2020 05:54 UTC
  • Vielelezo muhimu vya Uchaguzi wa Bunge nchini Syria

Tarehe 19 Julai, wananchi wa maeneo tofauti ya Syria walijitokeza kwenye maeneo ya kupigia kura kwa ajili ya kushiriki katika Uchaguzi wa Bunge.

Takwimu zinaonesha kuwa watu elfu nane walijitokeza kugombea viti katika bunge jipya la Syria lakini kati ya hao, ni 1658 wakiwemo wanawake 200 ndio waliokuwa wametimiza masharti ya kugombea.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Syria, watu waliotimiza masharti ya kupiga kura katika udhaguzi huo wa siku ya Jumapili walikuwa ni milioni 19. Wasyria waishio ndani ya Syria tu ndio waliokuwa na haki ya kushirki katika uchaguzi huo.

Hadi tunaandika uchambuzi huu wa kisiasa kulikuwa hakujatolewa takwimu rasmi ya kiwango cha watu walioshiriki kwenye uchaguzi huo lakini makisio ya awali yanaonesha kuwa karibu asilimia 50 ya wananchi wa Syria waliotimiza masharti wameshiriki kwenye uchaguzi huo. Idadi hiyo inahesabiwa kuwa ni kiwango kikubwa cha ushiriki wa wapiga kura hasa kwa kuzingatia kuenea ugonjwa wa COVID-19 na wasiwasi wa wananchi wa kukumbwa na kirusi hicho angamizi.

Ijapokuwa matokeo ya uchaguzi huo hayajatolewa, lakini inavyoonekana ni kwamba wafuasi wa chama tawala cha Baath ndio watakaopata ushindi mkubwa hasa kutokana na mafanikio aliyopata Rais Bashar al Assad katika kupambana na magenge ya kigaidi na kufanikiwa kuwafurusha magaidi katika sehemu kubwa ya ardhi ya Syria. Ikumbukwe pia kuwa bunge la Syria lina viti 250.

Rais Bashar al Assad akishiriki katika uchaguzi wa Julai 19, 2020 wa Bunge la Syria

 

Uchaguzi wa Bunge hilo linalojulikana kwa jina la "Majlis al Sha'ab" (Baraza la Wananchi) umefanyika katika majimbo 15 ya uchaguzi. Kiujumla uchaguzi huo ulikuwa na vielelezo kadhaa vilivyoupambanua na uchaguzi uliopita wa mwaka 2016. Kwanza jambo lililoleta mvuto katika uchaguzi huo wa Syria ambalo limeutofautisha na uchaguzi uliopita ni kwamba, maeneo yaliyofanyika uchaguzi huo wa juzi Jumapili yameongezeka sana. Sababu yake ni kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, jeshi la Syria limefanikiwa kuwafurusha magaidi na kukomboa sehemu kubwa ya ardhi ya nchi hiyo.  Tatizo kubwa linaloikabili Syria mbali na maeneo ambayo bado hayajakombolewa, ni ujenzi mpya wa nchi hiyo na ugumu wa maisha uliosababishwa na miaka mingi ya vita. Walid al Muallim, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema, uchaguzi huo ni ushindi mwingine kwa taifa hilo na utakuwa ni sababu ya kupungua uingilaji wa kigeni kama ambavyo utatia kasi pia mchakato wa kuijenga upya nchi hiyo ya Kiarabu.

Kielelezo cha pili kinahusiana na wagombea wa chama tawala cha Baath ambao wamepata nafasi ya kugombea kwa kuchaguliwa na wanachama, si kwa kuteuliwa na uongozi wa juu wa chama. Naam, mchujo wa wagombea hao umefanyika kwa kura za wananchi.

Wananchi wa Syria wameonesha kivitendo kuwa hawako tayari kuruhusu maajnabi wawaamulie mambo yao

 

Kielelezo cha tatu kinachoufanya uchaguzi wa siku ya Jumapili wa bunge la Syria uwe tofauti na uchaguzi uliopita wa miaka minne iliyopita ni kwamba uchaguzi huo umefanyika ndani ya utulivu na usalama takriban kamili. Ukitoa mkoa wa Dar'a, hakukuripotiwa uvunjaji wowote wa amani katika mkoa mwingine wowote wa Syria wakati wa kufanyika uchaguzi huo.

Taarifa zinasema kuwa, mkuu wa wilaya ya al Harak katika mkoa wa Dar'a alipigwa risasi na kuuliwa na magaidi wakati alipokuwa anakagua vituo vya kupigia kura mjini humo. Ikumbukwe kuwa Dar'a ndio mkoa ambao ulianza mgogoro wa Syria mwaka 2011. 

Suala la mwisho la kuligusia hapa ni kwamba ukiachilia mbali kiwango cha watu waliojitokeza kupiga kura na matokeo yake, suala lenyewe tu la kufanyika uchaguzi tena katika mazingira yenye changamoto chache sana hata za kiusalama, ni mafanikio makubwa kwa wananchi wa Syria na serikali yao. 

Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana wapinzani na maadui wa taifa la Syria wanafanya njama kubwa na wanatumia mbinu za kila namna kujaribu kuonesha kuwa uchaguzi huo si muhimu na wala si ushindi kwa taifa la Syria.