Erakat: Palestina imekuwa mhanga wa malengo ya uchaguzi ya Donald Trump
-
Saeb Erekat
Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) amesema kuwa Palestina imekuwa mhanga wa malengo ya uchaguzi wa Rais ya Donald Trump huko Marekani.
Saeb Erekat amesema kuwa, serikali ya Trump imedhihirisha tena jinsi inavyokiuka sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kuzihamasisha nchi mbalimbali kuitambua Quds inayokaliwa kwa mabavuu kuwa ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.
Erekat amesema kuwa, timu ya kampeni za uchaguzi ya Donald Trump inatumia mbinu mbalimbali na kuchukua hatua yoyote inayowezekana kwa ajili ya kushinda uchaguzi ujao wa rais wa Marekani hata kama hatua hiyo itavuruga au hata kuangamiza amani ya kimataifa.
Katibu wa Kamati ya Utendaji ya PLO ameitaka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na jinai na ukiukaji wa sheria wa utawala ghasibu wa Israel na wale wote wanaofunika na kuficha jinai hizo.
Saeb Erekat ametoa matamshi hayo baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza jana Ijumaa kwamba, Kosovo imekubali kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israe na kwamba Serbia pia imeahidi kuhamishia ubalozi wake katika mji mtakatifu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.